Na Helena Magabe – Tarime
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Tarime, Bashiri Abdalla Suleiman (Sauti), amesema kuwa mnamo Aprili 22, 2025, alipokea barua kutoka Tume Huru ya Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa mara ya pili mwaka 2025, barua ambayo inawataka waandikishe Mawakala wao katika daftari hilo, zoezi ambalo linatakiwa kuanza Mei Mosi hadi Mei 7, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Suleiman amesema anapenda kuuhabarisha umma kuwa CHADEMA haitashiriki katika mchakato huo kwa sasa, kutokana na msimamo wao wa “No Reform, No Election.” ameeleza kuwa chama hicho hakitapeleka mawakala kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 74, kifungu kidogo (1), hivyo iwapo kutatokea mtu yeyote akajiandikisha au kuapishwa kama wakala, chama chao hakitahusika.
“Kwa sasa tuna tume huru ya uchaguzi miongoni mwa mambo tunayo yalalamikia ni refoms kutoka Kwenye katiba kwenye tume ya uchaguzi Ibara 74 kifungu kidogo (1) kwa hiyo reforms hizo zikizungumzika kuwa tume huru ya uchaguzi ! tutashiriki kwa hiyo isije ikatokea kuna watu wakaenda kujiandikisha au kuapishwa wakarasimisha kuwa sisi hatutahusika ” alisema Suleiman
Ameongeza kuwa licha ya barua hiyo kuelekeza vituo 16 vya kujiandikisha katika kata 8 , CHADEMA haitashiriki katika kituo chochote. “Tunakiri kupokea barua hiyo, lakini hatutashiriki
” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Suleiman amezungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa Wilaya ya Tarime, na kuziomba mamlaka husika kuzitatua kwa haraka ili kuepusha athari zaidi. Miongoni mwa changamoto hizo ni uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa barabara katika maeneo kadhaa ya wilaya hiyo.