Latest Posts

TUNAHITAJI KURA ZA KUJAA KWA DKT. SAMIA OKTOBA 2025

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu (Oktoba 2025) kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kutokana na kuwa kiongozi imara katika kuwatumikia wananchi.

Mhe. Mbunge Njeza, amesema hayo wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kata ya Isuto na maeneo mengine jirani kwenye hafla ya kuwapongeza wenyeviti wanane waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji mwaka jana (2024) hivyo kufanya kata hiyo CCM kuibuka katika vijijini vyote na vitongoji 66 kati ya vitongoji 70 vya kata hiyo.

Kiongozi huyo, amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi na ya kimaendeleo kwa wananchi wake ikiwemo kwenye jimbo la Mbeya vijijini hivyo zawadi pekee ni kuipatia CCM kura za kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ambapo amegusia masuala ya elimu na afya kuwa kazi kubwa imefanyika.

Pia amesema kwenye barabara licha ya kuwa bado ni tatizo katika baadhi ya maeneo lakini Serikali imejitahidi na inaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara kila uchao ikiwemo barabara ya Mbalizi Shigamba ambayo tayari mkandarasi yupo eneo la mradi ili kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini Lameck Jilla amesema hoja za wapinzani kuwa hakuna kilichofanyika ni hoja mfu kwani miradi mbalimbali imetekelezwa na inaonekana kwa wananchi hivyo kutuma salamu zake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa CCM bado itashinda kwasababu bado ina nguvu na uwezo kuendelea kuwaongoza wa-Tanzania katika kulinda pia amani ya nchi.

Kwa upande wake mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Mbeya Mwal. Anthony Mwaselela, pamoja na kutoa pongezi zake kwa washindi wa Serikali za vijiji na vitongoji kupitia CCM amehimiza umoja na mshkamano ili kwenda kutatua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kushirikiana na viongozi wa ngazi za juu kwa utatuzi zaidi wa kero za wananchi.

Viongozi mbalimbali waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji mwaka 2024, wameshukuru kwa kuaminiwa na wananchi wao na kuahidi kuwa watumwa wao na kujenga ushirikiano baina yao na kuendeleza shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!