Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imekubaliana na mapingamizi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu juu ya kupinga uhalali wa notisi ya ushahidi wa ziada wa ACP Amini Mahamba katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu ambapo imesema notisi hiyo haikidhi sifa kwa mujibu wa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai(CPA)
Ikumbukwe jana Februari 23, 2026 upande wa Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga uliieleza mahakama juu ya notisi hiyo yenye ushahidi wa ziada wa ACP Mahamba ambae alikuwa kiongozi wa upelelezi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na walifahamu juu ya ushahidi huo wakati wanamuandaa kuja kutoa ushahidi Februari 16, 2026.
Akizungumza wakati wa kusomaa uamuzi huo mdogo Jaji Dunstan Ndunguru amesema kuwa Mahakama imezipitia hoja za jamhuri ambazo walizijenga kupita kifungu cha 308(1,2,3,4) na hoja za mapingamizi za Lissu ambazo alizijenga kupitia kifungu hicho hicho na mahakama imejiridhisha kwamba notisi hiyo haikidhi vigezo.
Jaji Ndunguru amesema “tunaona kwamba kifungu hicho kinafunguwa mlango wa kuletwa ushahidi wa shahidi ambae maelezo yake yalikuwepo lakini kwa bahati mbaya hayakusomwa wakati wa commital proceedings(mwenendo kabidhi) lakini hakifungui mlango wa kuleta ushahidi mpya ambao haukuwepo au haukuletwa au ambao umepatikana baadae wakati commital proceedings(mwenendo kabidhi) ilishafanywa.”
Mahakama imefafanua kuwa kwa mujibu wa Jamhuri na rekodi za mahakama ni kuwa shahidi ACP Mahamba maelezo yake yalishasomwa kwenye mahakama ya ukabidhi (Kisutu) na ushahidi ambao Jamhuri inataka kuuongeza ni wa yaliyopatikana wakati na baada ya uchaguzi mkuu hivyo haukidhi vigezo vya kifungu hicho cha 308 cha CPA.
Hatahivyo Mahakama imeenda mapumziko mafupi baada ya Jamhuri kuomba kutafakari maamuzi hayo madogo.