Na Jackison Gerald, Katavi
Kukosekana kwa utaratibu maalumu wa uzoaji taka wa muda mfupi katika baadhi ya masoko ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, kumetajwa kuwa changamoto inayowatia hofu wananchi kufuatia mlipuko wa mara kwa mara wa ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo yao.
Baadhi ya wakazi wa Mpanda wamesema licha ya changamoto hiyo kuwasilishwa kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, na matamasha mbalimbali, bado hakuna mfumo mzuri wa uzoaji taka wa haraka. Kwa mujibu wa wakazi hao, magari ya taka hupita mara moja kwa mwezi au zaidi, hali inayosababisha kujaa kwa taka sokoni, jambo linaloweza kuchochea maambukizi ya kipindupindu hasa kutokana na ongezeko la wafanyabiashara kwenye masoko hayo.
Wameiomba serikali kuweka utaratibu wa uzoaji taka angalau mara tatu kwa mwezi ili kukabiliana na hali hiyo, wakisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda afya za wananchi na kuzuia milipuko ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.