Baraza la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), chini ya Umoja wa Mataifa, limeamua kuwa Urusi inawajibika moja kwa moja kwa kuangushwa kwa ndege ya Malaysia Airlines, MH17, Julai 2014 mashariki mwa Ukraine, hatua inayohitimisha mjadala wa muda mrefu kuhusu tukio hilo la kusikitisha.
Kwa mujibu wa BBC, ndege hiyo ya abiria, iliyokuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur, ilianguka katika eneo la Donbas nchini Ukraine baada ya kudunguliwa kwa kombora la kijeshi lililotengenezwa na Urusi. Abiria wote 298 waliokuwa ndani waliuawa, wakiwemo raia wa Uholanzi (196), Australia (38), Uingereza (10), Malaysia, na Ubelgiji.
Kwa miaka mingi, Urusi imekuwa ikikanusha kuhusika na tukio hilo, lakini uamuzi wa ICAO sasa umeweka wazi kuwa nchi hiyo “ilishindwa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa” kwa kushindwa kulinda ndege ya kiraia dhidi ya mashambulizi ya silaha, kinyume na sheria za kimataifa za anga.
Kesi hiyo iliwasilishwa mwaka 2022 na serikali za Uholanzi na Australia, ambazo sasa zimeeleza kuridhishwa kwao na uamuzi wa baraza hilo.
“Tunatoa wito kwa Urusi hatimaye kukabiliana na wajibu wake kwa kitendo hiki cha kutisha cha vurugu na kulipa fidia kwa tabia yake mbaya,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Penny Wong.
Katika mwaka huohuo wa 2022, mahakama ya Uholanzi pia iliwapata na hatia ya mauaji raia wawili wa Urusi na M-Ukraine mmoja wanaoshutumiwa kuhusika na mashambulizi hayo, hata hivyo hawajakamatwa wala kutumikia kifungo cha maisha walichopewa.
Uamuzi wa ICAO unatarajiwa kuongeza presha ya kidiplomasia kwa Urusi, huku wafiwa na mataifa yaliyoathirika wakiendelea kusaka haki na fidia kwa familia za wahanga wa tukio hilo la kihistoria.