Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amekemea vikali hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ya kuweka ushuru wa asilimia 20 kwa bidhaa kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na ameahidi kuchukua hatua za kulipiza kisasi.
Trump ameiweka EU katika kundi la mataifa 60 yaliyoathiriwa na ushuru wa juu wa “ushuru wa kisasi” Jumatano, pamoja na China, India, Japan na Korea, huku mataifa mengine yakikumbwa na ushuru wa asilimia 10. Hatua hiyo ni mojawapo ya hatua kubwa zaidi za Marekani kuelekea sera ya ulinzi wa kiuchumi tangu Unyogovu Mkuu (Kushuka sana kwa uchumi wa dunia) wa miaka ya 1930.
Von der Leyen amesema ushuru huo wa Trump utakuwa na athari mbaya kwa walaji na wafanyabiashara ambao wamefaidika na biashara kati ya Marekani na Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Amehimiza EU kujihami dhidi ya madhara makubwa kwa biashara ya dunia yatakayosababishwa na hatua ya Trump ya kujitenga kiuchumi.
“Hakuna utaratibu katika machafuko haya. Hakuna mwelekeo wazi kupitia ugumu na sintofahamu inayoundwa, kwani washirika wote wa kibiashara wa Marekani wataathirika,” amesema katika taarifa ya moja kwa moja ya televisheni.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa EU itajiandaa na hatua za kujibu dhidi ya ushuru mpya wa Trump, pamoja na kifurushi cha euro bilioni 26 cha kulipiza kisasi kwa ushuru wa awali alioweka kwa chuma na alumini. Wakati huo huo, ameahidi kuwa Brussels (Mji wa Brussels nchini Ubelgiji- Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya) italinda viwanda vinavyokabiliwa na madhara makubwa zaidi.
“Tunakamilisha hatua ya kwanza ya kulipiza kisasi dhidi ya ushuru wa chuma, na sasa tunajiandaa kwa hatua zaidi ili kulinda maslahi yetu na biashara zetu iwapo mazungumzo yatashindikana,” amesema Von der Leyen akiwa Samarkand, Uzbekistan, ambako alikuwa akihudhuria mkutano.
“Tutafuatilia kwa makini athari zisizo za moja kwa moja za ushuru huu. Hatutakubali kuathirika na uwezo mkubwa wa uzalishaji duniani, wala hatutakubali bidhaa za bei ya chini kutupwa kwenye masoko yetu,” ameongeza, akirejelea uwezekano wa bidhaa za bei rahisi kutoka China na mataifa mengine ambayo sasa hayatapata soko la Marekani.
Von der Leyen ameonya kuwa hatua ya Trump ya kubomoa mfumo wa kimataifa wa biashara itaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi na biashara.
“Jumuiya ya raia milioni kadhaa itakabiliwa na gharama kubwa za vyakula. Dawa zitakuwa ghali zaidi, pamoja na gharama za usafiri. Mfumuko wa bei utaongezeka,” amesema na kuongeza, “Gharama za kufanya biashara na Marekani zitapanda kwa kiasi kikubwa”.
Hata hivyo, Von der Leyen hakutangaza hatua za moja kwa moja za kulipiza kisasi kwa niaba ya mataifa wanachama wa EU, lakini ameeleza kuwa mpatanishi wake wa biashara, Maroš Šefčovič, atakutana na mabalozi wa EU 27 Ijumaa ili kujadili hatua zinazofuata.
Trump, akizungumza katika Bustani ya Rose Garden ya Ikulu ya Marekani Jumatano, alieleza kuwa EU imekuwa ikinyonya uchumi wa Marekani kwa muda mrefu, na kuuita muungano huo “wa aibu” kwa tabia yake ya kibiashara.
“Sasa tutaipa Umoja wa Ulaya mzigo wake. Wana sheria kali sana, ni wafanyabiashara wagumu sana. Unadhani EU ni marafiki, lakini wanatunyonyoa. Ni jambo la kusikitisha sana kuona. Ni la aibu,” alisema Trump.
Trump alitangaza kuwa yuko katika hali ya dharura ya kitaifa kuweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa kutoka mataifa yote. Zaidi ya hayo, aliamua kuweka ushuru wa juu kwa takriban mataifa 60 ambayo Marekani inayaona kama “wahalifu wakubwa wa biashara.”