Jumuiya ya kijasusi ya Marekani imeitaja Urusi kama “tishio kubwa zaidi” kwa uadilifu wa uchaguzi nchini humo, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatatu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, taarifa hiyo imetiwa saini na taasisi kadhaa za kijasusi na usalama, zikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa (ODNI), Ofisi ya Shirikisho ya Upelelezi (FBI), na Wakala wa Usalama wa Mtandao na Miundombinu (CISA).
Kwenye tathmini hiyo, jumuiya hizo zimedai kuwa watu “wanaohusishwa na Urusi haswa” wanahusika katika kutengeneza video na makala za uwongo zinazolenga kudhoofisha imani ya wapiga kura kwa mchakato wa uchaguzi wa Marekani.
Inadaiwa kuwa maudhui hayo ya uongo yana nia ya kuwatia hofu wapiga kura kuhusu usalama wa mchakato wa uchaguzi, huku yakihamasisha maoni kwamba Wamarekani wanapaswa kushambuliana kwa misingi ya tofauti za kisiasa.