Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa anakubaliana na wazo la kusitisha mapigano nchini Ukraine, lakini ameweka masharti kadhaa magumu huku akisisitiza kuwa bado kuna “maswali yanayohitaji majadiliano”.
Putin alikuwa akijibu mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30, ambao Ukraine iliukubali mapema wiki hii baada ya mazungumzo na Marekani. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameuelezea msimamo wa Putin kama “ujanja wa kisiasa” na kutoa wito wa kuongezwa kwa vikwazo dhidi ya Urusi.
Wakati huo huo, Marekani imetangaza vikwazo vipya dhidi ya sekta ya mafuta, gesi na benki ya Urusi kama sehemu ya mashinikizo ya kumaliza mgogoro huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Moscow, Putin alisema:
“Wazo la kusitisha mapigano ni sawa, tunaliunga mkono, lakini tunahitaji kujadili baadhi ya masuala muhimu. Kusitishwa kwa mapigano kunapaswa kusababisha amani ya kudumu na kuondoa sababu kuu za mgogoro huu.”
Akaongeza kuwa huenda akawasiliana na Donald Trump, akisema: “Tunahitaji kujadiliana na wenzetu wa Marekani na washirika, labda nitapigiwa simu na Trump.”
Putin alihitimisha kuwa ingawa kusitishwa kwa mapigano kwa siku 30 kunaweza kuwa hatua nzuri kwa Ukraine, bado kuna mambo yanayohitaji makubaliano zaidi.