Latest Posts

UUZAJI ARDHI KIHOLELA PAWAGA: SERA NA SHERIA ZA ARDHI ZATOA MWELEKEO MPYA KUZUIA HASARA KWA WAKULIMA

Na Mwajuma Hassan – Iringa

Katika siku za hivi karibuni, Tarafa ya Pawaga wilayani Iringa imeshuhudia ongezeko kubwa la wananchi kuuza ardhi zao kiholela kwa wageni wanaovutiwa na fursa za kilimo cha umwagiliaji. Hali hii imezua sintofahamu miongoni mwa mamlaka za serikali na wadau wa maendeleo, hasa ikizingatiwa kuwa Pawaga ni eneo la kimkakati katika uzalishaji wa chakula, hususan zao la mpunga.

Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kupitia miradi mikubwa ya umwagiliaji kama Skimu ya Mkombozi na Magozi, yenye thamani ya shilingi bilioni 100, ili kuongeza tija katika kilimo cha mpunga.

Licha ya uwekezaji huu, baadhi ya wananchi bado wanauza mashamba yao kwa bei ya chini, wakikabiliwa na changamoto za kiuchumi na ukosefu wa uelewa juu ya athari za muda mrefu.

“Nilifikiri ni bora niuze nisaidie familia yangu, lakini sasa nasikia hii miradi italeta maendeleo makubwa. Inaniuma,” anasema Anna Kikoti, mkazi wa Pawaga.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kimataifa kuhusu Utawala Bora wa Umiliki wa Ardhi, Misitu na Uvuvi (VGGT) uliotolewa na FAO mwaka 2012. Mwongozo huu unalenga kuhakikisha kuwa umiliki na matumizi ya ardhi yanaendeshwa kwa uwazi, haki, na kwa manufaa ya jamii nzima, hususan wakulima na wanawake.

Kulingana na  Sera ya Ardhi iliyoboreshwa ya mwaka 1995 (toleo la 2023 )nchini Tanzania ,serikali imeweka vipaumbele mbalimbali vya kudhibiti uuzaji holela wa ardhi na kulinda ardhi ya kilimo.

Sera hiyo inasisitiza ushirikishwaji wa serikali za vijiji na halmashauri kabla ya kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi, na inahamasisha matumizi bora ya ardhi kupitia mipango shirikishi ya vijiji pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika miradi ya umwagiliaji kupitia vikundi vya uzalishaji.

Licha ya kuwepo kwa sera hizi, bado wananchi wa Pawaga wanaendelea kuuza maeneo yao kiholela bila kufuata utaratibu unaotakiwa.

Pia, Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 zinaelekeza bayana kuwa ardhi ya kijiji haiwezi kuuzwa kwa mtu binafsi au mwekezaji bila ridhaa ya serikali ya kijiji na baraza la ardhi. Uhamishaji wowote wa ardhi kwa watu kutoka nje ya kijiji lazima upitishwe na halmashauri ya wilaya.

Uuzaji usiozingatia sheria hizi unakiuka taratibu, na unaweza kusababisha migogoro ya ardhi, upotevu wa fursa za kiuchumi, na kuhatarisha usalama wa chakula kwa vizazi vijavyo.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa ardhi kutoka shirika la Landesa, Masalu Luhula, sera mpya imekuja kurekebisha mapungufu ya sheria zilizotangulia, hasa katika kulinda haki za wanawake na jamii zinazotegemea ardhi kwa maisha yao.

“Sheria za zamani hazikuwalinda ipasavyo wanawake. Mfano ni Tamko la Kimila la mwaka 1963 kuhusu usimamizi wa mirathi, ambalo limekuwa likiwaweka wanawake katika mazingira ya kunyimwa haki ya kumiliki ardhi. Sera iliyoboreshwa inalenga usawa wa kijinsia na usimamizi shirikishi wa ardhi,” alisema Masalu.

Masalu pia ameonya kuwa wawekezaji wengi hufanya mikataba ya moja kwa moja na wananchi bila msaada wa kisheria kwa upande wa wananchi, jambo linalowaweka katika hatari ya kupoteza rasilimali zao muhimu.

“Wawekezaji wanakuja wakiwa na wanasheria, lakini wananchi hawana msaada huo. Sera mpya italeta usawa iwapo itatekelezwa ipasavyo,” aliongeza.

Khadija Mrisho, Mratibu wa Kampeni ya Linda Ardhi ya Mwanamke, inayoendeshwa kwa ushirikiano wa mashirika 36 chini ya uratibu wa Landesa Tanzania , anasisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapewa haki sawa ya umiliki wa ardhi, hasa katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa kama Pawaga.

“Kumuwezesha mwanamke kumiliki ardhi ni sawa na kulinda usalama wa chakula kwa familia nzima, hasa maeneo ya kimkakati kama Pawaga.”

Hali ya sasa inadhihirisha kuwa wanawake wanapaswa kupewa kipaumbele ,si tu kwa kuwa ndio wazalishaji wakuu wa chakula, bali pia kwa sababu mara nyingi ndio waathirika wakuu wa migogoro ya ardhi na umaskini unaosababishwa na uuzaji holela wa ardhi.

Akizungumza hivi karibuni  katika hafla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa Skimu ya Magozi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, alitoa wito kwa wananchi kusitisha uuzaji wa ardhi kiholela:“Serikali inawekeza halafu watu wanauza maeneo yao kwa fedha ndogo. Wanazitumia, zinaisha, wanabakia kuwa masikini. Mashamba haya ni kwa ajili yako, watoto wako, wajukuu zako. Msifanye makosa haya.”

Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mkoa wa Iringa imetangaza mpango kabambe wa kupima kila kipande cha ardhi katika Tarafa ya Pawaga na kukiingiza kwenye mipango rasmi ya matumizi bora ya ardhi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema lengo kuu la mpango huo  ni kudhibiti uuzaji holela na kulinda ardhi kwa matumizi endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Kwa kuzingatia hilo, Shirika la Chakula Duniani (FAO) linashauri kuwa ardhi isimamiwe kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia maslahi ya wote, hasa wakulima na wanawake.

FAO haipingi uuzaji wa ardhi iwapo unafanyika kwa kufuata utaratibu wa kisheria, lakini inasisitiza kuwa:“Haki ya umiliki na matumizi ya ardhi iheshimiwe.”

FAO pia inaonya kuwa uuzaji wa ardhi usivunje haki za kimila, hasa za watu wa vijijini wanaotegemea ardhi kwa kilimo, malisho au misitu.

Ardhi ni uhai, si bidhaa .Hivyo ni wajibu wa serikali za vijiji, halmashauri, ofisi za ardhi, na asasi za kiraia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki zao, matumizi bora ya ardhi, na athari za uuzaji wa ardhi kiholela.

Ni dhahiri kuwa endapo sera na sheria za ardhi zitazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo, uuzaji wa ardhi kiholela Pawaga unaweza kudhibitiwa.

Ni wakati wa kulinda ardhi ya Pawaga kwa sasa, na kwa vizazi vijavyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!