Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Geita, Manjale Magambo, amewataka wanachama wa chama hicho kufuata utaratibu uliowekwa na chama, na kuacha tabia ya kuvuruga umoja wa chama hususan katika kipindi cha mchakato wa uchukuaji wa fomu za ubunge, udiwani, na uchaguzi wa ndani ya chama.
Magambo alitoa wito huo wakati wa ziara yake pamoja na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM mkoani humo, ambapo walitembelea Wilaya ya Bukombe, wakipita katika kata zote 122 za Mkoa wa Geita.
Amesema Chama Cha Mapinduzi bado kina nguvu na kinaamini kitavuka salama katika mchakato wa uchaguzi kutokana na maandalizi madhubuti yaliyofanyika. Alisisitiza kuwa michakato yote inapaswa kufanyika kwa amani, usawa, na kuzingatia taratibu, huku akionya kuwa hatakubali kuona chama kikivurugwa na watu wachache wasiopenda kuona nchi ikiendelea kuwa na amani.
Aidha, Magambo alibainisha kuwa chama kinatambua mchango wa baadhi ya wabunge na madiwani waliopo madarakani, na kwamba ni muhimu kuwapa nafasi ya kuendelea kutekeleza majukumu yao. Alionya kuwa hakuna mtu atakayevumiliwa endapo ataanzisha makundi au matabaka ndani ya chama.