Latest Posts

UVCCM MBARALI WATAJA SABABU ZA MITANO TENA CCM

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Katika kuadhimisha miaka 48 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, jumuiya ya vijana wa CCM (UVCCM) wilaya ya Mbarali umetembelea na kukagua mradi wa kituo cha kutibia maji Rujewa wilayani humo, kuzindua mashina ya chama hicho pamoja na kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika utunzaji wa mazingira.

UVCCM wilayani Mbarali umesema unaridhika na utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM katika wilaya hiyo ambapo umoja huo umewataka wananchi na wana CCM kuthamini mchango mkubwa wa CCM ambayo ndio chama tawala kinachoisimamia Serikali katika kuwatumikia wananchi.

Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Mbarali Medson Mwambapa, baada ya kuongoza ujumbe wa wilaya ya Mbarali na mkoa wa Mbeya kutembelea mradi huo wa kituo cha kutibia maji, amesema vijana na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla kinazo sababu lukuki za kuona kuwa mwenyekiti wa CCM Taifa ndugu Samia Suluhu Hassan bado anatosha na anastahili kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu (2025) kutokana na miradi mingi inavyotekelezwa.

“Kiukweli sisi wilaya ya Mbarali tunamshukuru Mungu, huu ni mradi mkubwa lakini pia tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mradi unakwenda kuokoa matatizo ya maji ambao ni matatizo makubwa kwenye jamii yetu na maji ni hitaji muhimu sana ambayo kwa miji yetu kama sasa inahangaika. Mradi wetu unaenda kugusa maeneo matatu, kuna Rujewa ambapo ndio kioo cha wilaya ambapo watu laki moja na themanini na tisa wanakwenda kunufaika, kuna Wanging’ombe watu laki mbili na ishirini na saba wanaenda kunufaika, na tuna Makambako watu laki moja na elfu tano wanaenda kunufaika na mradi huu ukiangalia jumla watu laki tano na ishirini na tatu na mia tano hamsini na nne wote watanufaika na mradi huu, ni kitu ambacho lazima tumshukuru Mhe. Rais”, amesema Mwambapa na kuongeza.

“Lakini kama vijana wa CCM tunajivunia sifa kwamba kwanini CCM inafaa au kwanini tunasema tunatakiwa tuendelee kupiga mitano tena nikama hivi, tunaona maendeleo ambayo tulikuwa tunatamani kuyaona hatukuweza kuyaona, cha msingi niwaombe wahandisi tumekuwa na changamoto sana ya kumaliza kwa wakati kwahiyo tupambane tumalize kwa wakati ili watu waanze kupata maji safi kwenye huu mradi mkubwa tuliouona”, ameeleza mwenyekiti huyo wa UVCCM wilayani Mbarali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mhandisi Kudra Yassin ambaye ni Meneja ufundi wa Mamlaka ya Maji Rujewa, mradi huo wa kituo kikubwa cha kutibia maji kutoka chanzo cha mto Mbarali, ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu 2025 na umegharimu mabilion ya fedha ikiwa ni za mkopo wa masharti nafuu kutoka nchini India.

Pamoja na hayo, UVCCM wilayani Mbarali wamepanda miti ya vimvuli katika shule ya sekondari Ihanga Mbarali na shule ya watoto wa dogo Mbarali (Mbarali English medium school), imezindua mashina manne ya wakereketwa wa chama hicho huku kikitathmini uhai wake wa miaka 48 na namna ya kuendelea kufanya kazi kama inavyotarajiwa na wananchi katika kuendelea kuisimamia Serikali.

Maadhimisho ya kitaifa ya miaka 48 ya CCM yanatarajiwa kufanyika Februari 05, 2025 jijini Dodoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!