Na Josea Sinkala, Songwe.
Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UVCCM) mkoa wa Songwe umesema unasikitishwa na baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani wanavyopelekeshwa na viongozi wao wa ngazi za juu.
Hii ni kutokana na kudaiwa kuwa vijana hao wanatambua kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita lakini hawawezi kutoka hadharani kutokana na viongozi wa ngazi za juu ya vyama vyao.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wa CCM mkoa wa Songwe Bi. Fatuma Hussein Mnahwate, wakati akizungumza kwenye kikao cha mafunzo ya kamati za utekelezaji kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 kilichofanyika Mlowo wilayani Mbozi kwa kuwakutanisha wenyeviti na makatibu wa wilaya zote za mkoa huo na kamati zao ambapo amezungumza hayo bila kuwataja moja kwa moja wapinzani hao.
Ujio wa matamshi haya ya mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Songwe yanakuja kufuatia vijana wa CHADEMA mkoani Songwe na Chama Cha ACT Wazalendo mkoani humo kudai hawana makubaliano yoyote na UVCCM wala CCM kuwa watamuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa mwaka huu 2025 kupitia CCM kama ilivyodaiwa na mwenyekiti wa UVCCM mkoa huo kuwa wapinzani hasa vijana wamekubaliana na UVCCM kumuunga mkono Rais Samia kwenye uchaguzi huo.
Katika kikao hicho wajumbe hao wamepata elimu mbalimbali zihusuzo jumuiya ya vijana na chama cha Mapinduzi kwa ujumla ikiwemo kutoka kwa katibu mwenezi wa CCM mkoa mwalimu Yusuph Ally Rajabu.
Akizungumza na viongozi hao wa vijana, mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbozi Majaliwa Mlawizi kwa niaba ya mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa kutoka mkoani Songwe (MNEC) Ndugu Aden Mwakyonde, amewataka viongozi hao kuendelea kuwa jumuiya imara katika kukilinda Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake ili kuzidi kuwatumikia wananchi na kuwavuta walioko nje ya CCM kujiunga na CCM kutoka vyama vingine na kwa wasio na vyama.
Pamoja na hayo MNEC huyo wa mkoa wa Songwe, ameahidi kuchangia mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya kuwaunga mkono vijana hao kwenye ujenzi wa nyumba ya katibu wa wilaya, na kuwataka kuendelea kushirikiana kufanya kazi ya Chama hicho.
Naye mjumbe wa Baraza kuu la vijana wa CCM Taifa akiwakilisha mkoa wa Songwe Shaibath Kapingu, amewataka vijana kutokubali kuwa machawa na wapambe wa watu na kuharibu taswira njema ya chama na viongozi walioko madarakani na kwamba wakati wa kugombea nafasi mbalimbali ukifika kila mwanachama ataruhusiwa kuomba kugombea.
Pia amehimiza vijana kujiandaa na uchaguzi huo kwa kuhakikisha pia wanagombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwatumikia wananchi.