Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba ili kuboresha huduma katika hospitali, vituo vya afya, na zahanati.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Wizara ya Afya imenunua mashine za ultrasound 457, na hivyo kufikisha idadi ya mashine 970 zilizogawiwa kwenye hospitali mbalimbali, zikiwemo Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalum, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo, Oktoba 9, 2024, jijini Arusha alipokuwa akifungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wana Radiolojia Tanzania (TARA), lenye kaulimbiu inayosema “Tafsiri ya Majibu ya Vipimo na Maadili (Pattern Recognition and Ethics).”
Akizungumzia zaidi kuhusu uwekezaji huo, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imenunua mashine za kidigitali za x-ray 386, hivyo kufikia jumla ya mashine 469 zilizopo katika hospitali mbalimbali nchini. Aidha, Serikali imenunua mashine saba mpya za MRI, na kufikisha mashine 13 zilizopo katika hospitali za umma. Vilevile, mashine za CT scan zimewekwa katika kila mkoa nchini.
“Kama Mhe. Rais asingefanya uwekezaji huu mkubwa, ni fedha ngapi zingeenda kutumika nje ya nchi? Lakini vifaa peke yake haviwezi kutoa matokeo, ni nyinyi wataalamu ndiyo mnaotoa huduma, kwa hiyo tunawashukuru sana na tunatambua mchango wenu,” amesema Dkt. Biteko.
Serikali inajikita katika kuimarisha sekta ya afya, pamoja na miundombinu na maji, ili kuleta ustawi wa Watanzania. Dkt. Biteko amewataka wataalamu wa radiografia kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanaiheshimu na kuilinda taaluma yao.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya, ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi. Amesema Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imepata mashine ya kisasa ya PET-CT kwa uchunguzi wa awali wa saratani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kuwa serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 72 kwa ajili ya vifaa tiba na ujenzi wa hospitali katika mkoa wake, na amemshukuru Rais Samia kwa miradi mikubwa ya umeme inayoendelezwa, kama vile Bwawa la Julius Nyerere.