Vatican imetoa picha ya kwanza ya Papa Francis tangu alipopelekwa hospitalini mwezi mmoja uliopita, akiendelea kupokea matibabu kutokana na nimonia.
Picha hiyo inamuonesha Papa akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu mbele ya madhabahu katika Hospitali ya Gemelli, Rome, ambako amekuwa akipata nafuu.
Mapema Jumapili, Papa Francis aliwashukuru waumini wote waliomtakia mema kwa maombi yao na akawaombea amani wale walioko katika nchi zilizoathiriwa na vita.
Hiyo ni Jumapili ya tano mfululizo ambayo Papa hakuhudhuria ibada kanisani. Vatican iliripoti mapema wiki hii kwamba X-ray imethibitisha hali yake inazidi kuimarika, ingawa bado anahitaji kuendelea na matibabu hospitalini.