Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Jokate Urban Mwegelo amewasilisha mapendekezo muhimu kwa niaba ya vijana wa kutoka vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika ikiwemo pendekezo la kuwa na Tamasha kubwa la Vijana wa nchi za vyama vya ukombozi yaani (Liberations Movement Youth Festival), litakalokutanisha vijana wa nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe, Angola na Namibia ili wafanye mijadala, kubadilishana uzoefu na fursa za kiuchumi ambapo pendekezo hilo limekubaliwa.
Jokate ametoa mapendekezo hayo kwenye mkutano mkuu maalum wa vyama sita rafiki vya ukombozi kusini mwa Afrika uliofanyika mjini Guten nchini Afrika Kusini uliokutanisha Marais wa nchi za ukombozi Kusini mwa Afrika na vyama vyao ukiongozwa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na kuratibiwa na Katibu Mkuu wa ANC Fikili Mbalula ambapo Rais Samia amewakilishwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda.

Jokate amesema “Ninawashukuru sana viongozi wenzangu wa vyama vya ukombozi kwa heshima kubwa ya kunichagua kuwawakilisha vijana wa vyama vyote vya ukombozi Kusini Mwa Afrika kuwasilisha mapendekezo ya vijana kwa vyama vyetu hivi na hivyo kunipa fursa ya kuzungumza mbele ya wanamajumui wa heshima na wageni kutoka Mataifa mengine nje ya Afrika.
Jokate amewasilisha pia mapendekezo ya vijana juu ya utekelezwaji wa sera za kina za vijana ili kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa elimu bora, mafunzo ya ufundi stadi, ushauri, ajira, fursa za kiuchumi na njia za uongozi, pamoja na kutoa mapendekezo yake kwa kushawishi mkutano huo kukubali kufanyika kwa tamasha kubwa na la kihistoria la vijana wa nchi za vyama vya ukombozi yaani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na fursa za kiuchumi.

“Kwa heshima kubwa na moyo ni furaha iliyoke Kwamba pendekezo hili limekubaliwa na hivyo imebaki utekelezaji, asanteni kwa Imani kubwa mlionionesha vijana wenzangu wa Afrika”, ameeleza.
Jokate Urban Mwegelo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amewakilisha vijana wa vyama vya ukombozi katika Mkutano huo ambavyo ni CCM (Tanzania), ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola), SWAPO (Namibia), ZANU PF (Zimbabwe) pamoja na FRELIMO (Msumbiji).
Mkutano huo ulioanza Julai 25 na kumalizika Julai 28, 2025 katika mji wa Gauten, Afrika Kusini umekuwa na dhima kuu ya kutetea mafanikio ya ukombozi, kusukuma maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi, kuimarisha mshikamano kwa ajili ya Afrika bora pamoja na kutambua jukumu la kimapinduzi na muhimu lililofanywa na vijana katika harakati za ukombozi kwa kuwajumuisha vijana katika hatua zote muhimu za harakati za kisiasa na maendeleo ya jamii kama washirika sawa katika kutumia ubunifu, uvumbuzi na nguvu zao.