Latest Posts

VIONGOZI WA DUNIA WAMLILIA PAPA FRANCIS: MJUMBE WA HURUMA NA AMANI

Kifo cha Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki aliyefariki Jumatatu akiwa na umri wa miaka 88, kimezua maombolezo makubwa duniani kote. Viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii kutoka kila pembe ya dunia wametoa salamu zao za rambirambi, wakimkumbuka kama kiongozi wa kiroho mwenye huruma, msimamo thabiti kwa wanyonge na mpenda amani wa kweli.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitoa heshima kwa Papa Francis, akimkumbuka kwa mchango wake wa kipekee katika kutangaza matumaini, hasa kwa maskini.

“Kuanzia Buenos Aires hadi Roma, Papa Francis alitaka Kanisa liwe chanzo cha furaha na matumaini kwa maskini. Aliunganishwa watu na mazingira. Matumaini hayo na yaendelee kuishi hata baada ya yeye kututoka,” alisema Macron katika taarifa yake rasmi.

Friedrich Merz, Kansela mtarajiwa wa Ujerumani, alisema ameguswa sana na kifo cha Papa, akimtaja kama mtu aliyekuwa sauti ya haki. “Kifo cha Papa Francis kimenisikitisha sana. Atakumbukwa kwa juhudi zake zisizoisha kwa ajili ya wanyonge, haki na upatanisho,”

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alitoa ujumbe wa rambirambi, akimwelezea Papa kama kiongozi aliyevuka mipaka ya dini. “Aliongoza kwa unyenyekevu na upendo wa kweli kwa wasiojiweza. Aliwasha nuru ya matumaini kwa mamilioni, hata zaidi ya Kanisa Katoliki”.

Rais wa Israeli Isaac Herzog ameeleza masikitiko yake kwa kifo cha Papa, akimkumbuka kama mjenzi wa maelewano ya kidini. “Natoa pole kwa jumuiya ya Kikristo. Papa Francis alikuwa mtu wa imani ya dhati na huruma isiyo na mipaka. Aliona umuhimu wa kukuza uhusiano na dunia ya Kiyahudi na kuendeleza mazungumzo ya imani mbalimbali,” alisema Herzog.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alimtambua Papa Francis kama kinara wa maelewano ya kidini na binadamu. “Ametuachia pengo lisilozibika. Alisimama kwa ajili ya amani, mshikamano wa kidini na utu wa wote,” alisema.

Ikulu ya Marekani ilitoa ujumbe mfupi kupitia jukwaa la X (zamani Twitter), ikiwa na picha za Rais Donald Trump na Makamu wa Rais JD Vance walipokutana na Papa Francis, ikisindikizwa na maneno “Rest in Peace.” Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, aliyekutana na Papa Francis siku ya Jumapili, saa chache kabla ya kifo chake, alishiriki hisia zake za huzuni:

“Nimehuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Papa Francis. Nilikuwa na furaha kumuona jana, ingawa alikuwa mgonjwa sana. Nitamkumbuka hasa kwa mahubiri yake ya mapema wakati wa janga la COVID, yalikuwa ya kuvutia sana,” amesema Vance.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!