Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Kenya wamelaani vikali ghasia zilizozuka katika Eneo Bunge la Kilgoris, Kaunti ya Narok, kati ya wananchi na maafisa wa polisi kuhusu mgogoro wa ardhi ya ekari 6,800 – ambapo watu watano waliuawa.
Katika taarifa ya pamoja iliyosainiwa na Kiongozi wa Chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri wa zamani Mithika Linturi (Kilimo), Justin Muturi (Utumishi wa Umma), Kiongozi wa Chama cha DAP-K Eugene Wamalwa na Katibu Mkuu wa zamani Torome Saitoti, imeelezwa kuwa tukio hilo ni sehemu ya mwelekeo hatari wa vurugu zinazofadhiliwa na serikali.
Wakimshutumu Rais William Ruto, viongozi hao walisema utawala wake umejikita katika kunyakua ardhi za wananchi kwa mabavu, wakitoa mfano wa visa vya awali vya Mavoko, Nairobi na Ndabibi vilivyoandamwa na migogoro ya ardhi.
Viongozi hao wamesema kuwa wapo tayari kufikisha kesi hizo za ukiukwaji wa haki za binadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ili kuhakikisha haki inapatikana.
“Kwa historia ya Ruto ya kuwahamisha watu kwa nguvu, tunataka kumkumbusha kuwa matendo haya ni uhalifu dhidi ya binadamu. Tumejipanga kuyapeleka mashitaka haya ICC,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Wamesema kuwa vyombo vya usalama nchini na taasisi huru kama Mamlaka ya Uangalizi wa Polisi Huru (IPOA) na Idara ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) zimegeuzwa kuwa silaha za serikali kufunika maovu.
“Tunashuhudia kuibuka kwa utawala wa kihuni usioheshimu maisha ya binadamu, usiotii sheria na usiozingatia Katiba ya nchi yetu,” wameongeza.
Viongozi hao pia walizungumzia mchakato wa uteuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa wasiwasi, wakidai kuwa mchakato huo hauaminiki.
Wamedai kwamba ili kuleta imani kwa Wakenya na wadau wote, mashauriano na vyama vya upinzani yahusishwe kabla ya uteuzi wa makamishna wa IEBC.
“Kushindwa kuunda tume ya uchaguzi yenye kuaminika kunaweza kuweka msingi wa uchaguzi wa 2027 uliojaa dosari, jambo ambalo Wakenya hawatakubali kamwe.”