Latest Posts

WAAJIRI WATAKIWA KUWARUHUSU WAKUU WA IDARA KUHUDHURIA KIKAO KAZI DODOMA

Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, amewataka waajiri wote nchini kuhakikisha wakuu wa idara za utawala na usimamizi wa rasilimali watu wanahudhuria kikao kazi cha mwaka kwa ajili ya kujifunza mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 12, 2024, jijini Dodoma, Daudi amesema kikao kazi hicho kimepangwa kufanyika kuanzia Desemba 17 hadi 19, 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma, eneo la Mtumba. Amewahimiza washiriki kufika tarehe 16 Desemba kuanzia saa 10:00 jioni kwa ajili ya kuchukua vitambulisho na nyaraka muhimu za kikao.

Daudi ameeleza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu na kutoa maelekezo kuhusu usimamizi wa rasilimali watu kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa. Mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali kama vile e-Watumishi, e-Uhamisho, e-Utendaji, e-Mrejesho, na HR Assessment.

“Nawasihi waajiri wote waruhusu wakuu wa idara kushiriki kikamilifu kwenye kikao kazi hiki ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali watu, kuboresha utoaji wa huduma, na kupunguza malalamiko ya wananchi,” amesema Daudi.

Pia ametoa wito kwa washiriki wote kujisajili kupitia mfumo wa kidijitali wa https://tsms.gov.go.tz kabla ya Desemba 13, 2024, ili kushiriki kwenye kikao hicho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma, Felister Shuli, amesisitiza umuhimu wa rasilimali watu katika maendeleo ya sekta nyingine. Amebainisha kuwa mifumo bora ya usimamizi wa rasilimali watu ni msingi wa kuongeza ufanisi wa taasisi, kupunguza urasimu, na kuimarisha ubora wa huduma kwa wananchi.

Kaulimbiu ya kikao kazi hicho ni “Kusimamia Sera na Sheria za Utumishi wa Umma Kupitia Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala ya Kidijitali Iliyoimarishwa.” Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!