Latest Posts

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA UKWELI

Na Helena Magabe – Tarime

Waandishi wa habari wametakiwa kuhakikisha wanatoa taarifa za kweli na za kuaminika kwa jamii, kwani bado hawajaonyesha juhudi za kutosha katika kuhakikisha kuwa taarifa wanazotoa ni sahihi na zinafaa kutumiwa. Ingawa dhana ya ukweli haiepukiki, bado ni changamoto kuitafsiri kwa usahihi.

Wito huo umetolewa Aprili 10, 2025, katika semina iliyofanyika katika mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, Nyamongo. Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Godfley Kalago, ambaye pia ni mwandishi wa habari kitaaluma, aliwaeleza waandishi hao kuhusu hali ya kuporomoka kwa maadili ya uandishi wa habari, akisisitiza kuwa tafsiri ya ukweli hutegemea mitazamo ya watu, lakini habari lazima ziwe za kweli ili zitumike ipasavyo.

Kalago amewasisitizia waandishi wa Mkoa wa Mara umuhimu wa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuepuka kuibua migogoro isiyo ya lazima katika jamii.

Amesema kuwa maendeleo huambatana na changamoto, lakini ni jukumu la mwandishi kutathmini kwa makini hali halisi ya jamii, kuelewa mahitaji na maslahi ya wananchi, na kujitolea kufuatilia habari kwa kutumia nyenzo zinazotolewa na vyombo vyao vya habari.

Aidha, amehimiza waandishi hao kuwa na ushirikiano mzuri na wananchi wa kawaida, kufahamu athari za habari katika mchakato wa maendeleo, na kuwa na ujuzi, utambuzi na uzoefu katika masuala wanayoyaripoti.

Baadhi ya waandishi wameeleza changamoto wanazokumbana nazo, zikiwemo kuwekewa mipaka na wadau kuhusu wanachopaswa kuandika, kutopata ushirikiano kutoka kwa baadhi ya vyanzo muhimu vya habari, na kunyimwa taarifa muhimu kwa manufaa ya umma.

Ghati Msamba, mwandishi wa gazeti la Uhuru, amesema kuwa semina hiyo itawasaidia waandishi kuandika habari za maendeleo kwa ufanisi zaidi. Aliwataka wananchi kutokuwa wabishi wanapoletewa miradi ya maendeleo na serikali, bali waiunge mkono badala ya kutoa visingizio visivyo na msingi, hali ambayo huzuia ukuaji wa uchumi.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Mugini Jacob, aliishukuru kampuni ya Barrick kupitia makao makuu yake jijini Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Barrick North Mara katika kuandaa mafunzo hayo.

Amesema mafunzo hayo yatawaimarisha waandishi wa Mkoa wa Mara katika kuandika habari za kweli na zinazohamasisha maendeleo.

Meneja wa Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, amesema waandishi wa habari wa Mkoa wa Mara wamekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia mabadiliko, hasa kwa kuwasaidia waliokuwa wavamizi wa mgodi kutafuta kazi mbadala.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kipindi cha mvua kimewafanya baadhi yao kurejea vitendo vya awali.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinaly Lyambiko, amesema kuwa hakuna mtu mkamilifu, na kwamba wakati mwingine mwandishi huandika habari kuhusu jambo ambalo bado halijatekelezwa, lakini hiyo huwa njia ya kufikisha ujumbe kwa wahusika.

“Mtu akiandika habari kwenye gazeti kuhusu jambo ambalo hatujalitekeleza kwa sasa, hiyo ni njia ya kuwasilisha ujumbe – na sisi hutekeleza. Tunawashukuru kwa sababu mafunzo kama haya hutujenga na kutuboresha,” alisema Meneja Lyambiko.

Waandishi hao pia wanatarajiwa kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha afya kilichopo Kata ya Nyarukoba, Kijiji cha Genguru, ili kujionea jitihada za maendeleo zinazofanywa na mgodi huo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kwa vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!