News, Njombe.
Wafamasia kanda ya nyanda za juu kusini wameiomba serikali kuondoa kigezo cha mtihani wa sekretarieti ya ajira kwa kada hiyo zinapotangazwa nafasi za kazi badala yake ajira ziweze kutolewa kwa vigezo vya chuo wanavyotoka kuliko kufanya mitihani ambayo imekuwa ikiwanyima fursa vijana wenye uwezo wa kazi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafamasia (PCT) kanda ya Nyanda za juu kusini Jackson Nzinza ameeleza hayo akiyataja kama miongoni mwa maoni yaliyotolewa na wanachama wa chama hicho mkoani Njombe kuelekea mkutano mkuu wa mwaka unaotarajiwa kufanyika mkoani Arusha.
“Wanachama wamependekeza na kuiomba sekretarieti ya ajira kuwa zinapotangazwa ajira basi mfamasia aajiriwe kwa vile vigezo ambavyo chuo kilimwamini badala ya kufanyishwa mtihani, wanasema unakuta mtu amesoma miaka minne na akaenda kwenye mafunzo ya kazi halafu uje kumtathmini kwa mtihani unakuwa umemuonea”, amesema Nzinza.
Amesema wakati wa usahili inaweza kutokea mtu mwenye vigezo na uwezo mkubwa wa kufanya kazi akaweza kusahau kitambulisho sehemu aliyopumzika na kusababisha kukosa nafasi aliyoitarajia kwa muda mrefu.
Aidha amesema wanachama wa chama hicho wameishauri serikali kuongeza vigezo vya mwanafunzi kusoma kozi ya famasia badala ya kuwa na kigezo cha D mbili kwa kuwa taaluma hiyo kwa sasa imeshushwa thamani.