Latest Posts

WAHIFADHI WAPINGA MAUAJI YA WANYAMAPORI NAMIBIA KULISHA RAIA, WATOA ONYO LA HATUA ZA KISHERIA

Wataalamu wa uhifadhi, wanasayansi, na watafiti katika nchi za Kusini mwa Afrika hususan Namibia, wameonya kuchukua hatua za kisheria ili kusitisha mauaji ya wanyamapori kama “mkakati wa kupunguza njaa.”
 
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), njaa imeathiri watu takriban 700,000 nchini Namibia, hasa katika maeneo ya vijijini, na hali hiyo imezidi kuwa mbaya kutokana na ukame unaoikumba kanda hiyo ya Kusini mwa Afrika.
 
Mamlaka nchini Namibia zimeanza kutekeleza mpango wa kuua baadhi ya wanyamapori kwa lengo la kuokoa makundi mengine na mazingira yao. Nyama itakayopatikana itagawiwa kwa jamii zilizoathirika zaidi na njaa.
 
Mpango huo ulioanza Agosti 14, unalenga kuua wanyama 723, wakiwemo viboko 30, nyati 60, swala 50, nyumbu wa buluu 100, pundamilia 300, tembo 83, na swala wa eland 100.
 
Hata hivyo, uamuzi wa baraza la mawaziri la Namibia kuagiza wizara ya mazingira kusaidia juhudi za serikali kupambana na ukame, umekosolewa vikali na wataalamu wa uhifadhi, na umeibua mjadala mkubwa kimataifa.
 
Hatua hiyo pia imegawa maoni ya umma kuhusu muda wa uamuzi huo na utaratibu wa kutekeleza mauaji hayo na kugawa nyama kwa jamii zilizoathirika.
 
Akizungumza na Kituo cha Habari cha VOA, Mtaalam wa uhifadhi, Izak Smit, amesema kuwa katiba ya Namibia inalinda urithi wa wanyamapori wa asili, na mpango wa mauaji unaweza kuwa na athari mbaya kwa uwiano wa wanyamapori katika mazingira yao.
 
“Ni kitendo kisichowajibika kufanya hivyo baada ya ukame na kabla ya msimu wa mvua, wakati ambapo wanyama wanahitaji kuzaana ili kurejea katika hali ya kawaida baada ya ukame,” alisema Smit.
 
Wapinzani wa mpango huo wameonya kuwa watakimbilia mahakamani kama mamlaka za Namibia hazitasitisha mauaji hayo, wakidai kuwa mpango huo ni hatari kwa rasilimali za asili za nchi, hauna uendelevu, hauna uhalali, na hauna msingi wa kisayansi.
 
Herbert Jauch wa Shirika la Haki za Kijamii na Kiuchumi, alisema kuwa mahakama inaweza kuwa siyo jukwaa sahihi la kutatua mgogoro huo, ambao unaonekana kujikita katika hitaji la kulinda tembo wa Namibia ambao ni kivutio kikubwa cha utalii na urithi wa wanyamapori nchini humo.
 
Msemaji wa Wizara ya Mazingira ya Namibia, Romeo Muyunda, amesema mpango huo wa mauaji umechukuliwa nje ya muktadha, na tembo wa jangwani wa Namibia si sehemu ya tembo walengwa.
 
“Tuna wanyamapori zaidi ya milioni 3 nchini, hivyo hao 723 hawafikii hata asilimia 1 ya jumla ya wanyama wetu,” amesema Muyunda.
 
Nyama itakayopatikana kutokana na mauaji hayo itahifadhiwa katika viwanda mbalimbali vya kusindika nyama nchini na itagawiwa kupitia mpango wa misaada ya ukame. Ofisi ya Waziri Mkuu itaongoza juhudi hizo kwa kushirikiana na wizara nyingine ili kukabiliana na ukame na njaa nchini.
 
Mpango wa mauaji hayo umeibua mjadala mkubwa kimataifa, huku wataalamu wa uhifadhi wakihofia kuwa unaweza kuweka mfano mbaya kwa nchi nyingine za Afrika ambazo hazina mafanikio sawa katika uhifadhi kama Namibia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!