Na Josea Sinkala, Mbeya.
Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imefanya kikao cha ushauri wilaya (DCC) na kupokea maoni mbalimbali katika kuboresha huduma na miradi ya maendeleo wilayani humo.
Wakichangia kwa nyakati tofauti kwenye kikao hicho, wajumbe wameshauri na kuihoji Serikali sababu za kusuasua kwa baadhi ya miradi ikiwemo barabara ya Isyonje Kikondo Makete ambayo kwa Mbeya bado hatua hazionekani kuanza kwa ujenzi licha ya kupigiwa kelele mara kwa mara ikiwemo na Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza.
“Barabara ya Isyonje Kikondo imekuwa na maeneo ambayo magari yanakwama kabisa sasa watu wa TANROADs wanatusaidiaje ili tusiwe tunakwama ikizingatiwa kwa sasa ndio tunatoa viazi na uchumi uko kule”, amehoji mjumbe wa kikao hicho bwana Gerald Shayo, kaimu afisa maliasili wilayani Mbeya.
Akijibu hoja hiyo, kaimu meneja wa wakala wa ujenzi wa barabara Tanzania (TANROADs) mkoa wa Mbeya Mhandisi Nicodemus Kalenzo, amesema barabara hiyo ilishaanza kujengwa kutoka Makete mkoani Njombe lakini TANROADs ilishaandika barua kwenda makao makuu kwa ajili ya kuomba kupata mkandarasi mwingine atakayeanzia kazi mkoani Mbeya na kwa sasa wanasubiri kujibiwa barua yao na kuwahakikishia wananchi kuwa barabara hiyo itajengwa ikiwa ni pamoja na barabara nyingine katika kata ya Ilungu zilizohojiwa na afisa mtendaji kata ya Ilungu.
Pia wamehimiza kuharakishwa kwa ujenzi wa barabara ya Mbalizi Shigamba ambayo imearifiwa kuwa tayari mkandarasi yupo eneo la mradi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kuanza na kilomita mbili ambazo tayari fedha zimekwishatolewa.
Pia wajumbe hao, wameshauri kutilia maanani suala la utunzaji mazingira ili kutunza vyanzo vya maji na uimarishaji vyanzo vya mapato ili kuwa na ukusanyaji bora zaidi wa mapato bila kuwaumiza walipa kodi.
Katika kikao hicho taasisi mbalimbali za Serikali zimewasilisha kazi zilizofanyika kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2024 wakiwemo wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA), shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mbeya na wakala wa maji vijijini (RUWASA).
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya Gideon Mapunda, amewasilisha pia taarifa ya Halmashauri ambapo pamoja na miradi mingine iliyotekelezwa pia Halmashauri hiyo imepitisha makadirio ya bajeti ya jumla ya shilingi billion sitini na sita ya kukusanywa na kutumiwa wilayani humo.
Kikao hicho kiliongozwa na mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Morris Malisa ambaye amesisitiza watumishi hasa wakuu wa idara kila mmoja kuendelea kusimama ipasavyo katika eneo lake kufanya kazi kwa weledi kwa maslahi ya umma ili kumaliza miradi kwa wakati ikiwemo suala la elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wote wanaopaswa kuwa shuleni wanaenda kusoma na kuahidi kusimamia suala la uhifadhi wa mazingira ili kutunza vyanzo vya maji