Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Elipidius Baganda, amewahimiza walimu wakuu kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu ya kujitegemea wakiwa shuleni.
Ametoa wito huo alipokuwa akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule kwa walimu wakuu wa Mkoa wa Singida, iliyofanyika tarehe 13 Oktoba 2024.
Dkt. Baganda ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya maboresho ya mtaala wa elimu ili wanafunzi wapate maarifa ya amali yatakayowawezesha kujiajiri na kujipatia kipato baada ya kuhitimu.
“Maisha ni kazi; wanafunzi wanapaswa kufundishwa kufanya kazi na kujitegemea. Kila shule inapaswa kuwa na mradi wa EK (Elimu ya Kujitegemea). Hakikisheni hili linafanyika, na tutafuatilia kuona kama miradi hiyo imeanzishwa katika shule zote za Mkoa wa Singida,” alisema Dkt. Baganda.
Aidha, amewataka walimu wakuu kuyatekeleza mafunzo waliyoyapata kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za shule, hususani kwenye miradi ya ujenzi, ili fedha zinazotolewa na Serikali zitumike kwa tija inayokusudiwa.
Jumla ya walimu wakuu 643 kutoka Mkoa wa Singida wamepatiwa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule, ambapo walifundishwa kuhusu uongozi bora, uandaaji wa mipango ya maendeleo ya shule, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, ustawi na usalama wa wanafunzi, usimamizi wa miundombinu, na ushirikishwaji wa jamii.
Mafunzo haya ni sehemu ya awamu ya tatu ya mafunzo yanayoendelea katika mikoa 13 ya Tanzania Bara, yakihusisha walimu wakuu 8,551. Mafunzo hayo yanaendeshwa na ADEM chini ya mradi wa BOOST, ukiwa na lengo la kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule, na hivyo kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.