Chama cha Walimu Wilaya ya Geita kimeanzisha mpango wa kuwawezesha walimu wanawake kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, lengo likiwa ni kuwaongezea vipato vyao vya ziada na kuwaepusha na utegemezi wa mikopo yenye masharti kandamizi.
Akizungumza katika kikao cha walimu wanawake kilichofanyika hivi karibuni, Katibu wa CWT Wilaya ya Geita, Kibibi Lukindo, alisema wengi wa walimu wamekuwa wakikumbwa na changamoto za kifedha kutokana na kukosa maarifa ya uendeshaji wa miradi ya kujikimu.
Kwa upande wao, baadhi ya walimu wanawake walioshiriki kikao hicho wameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuwa na vyanzo mbadala vya mapato tofauti na mshahara wa kila mwezi, hivyo kuimarisha maisha yao na ya familia zao.
Mbali na utoaji wa mafunzo hayo, chama hicho pia kimetoa majiko ya gesi kwa baadhi ya walimu wanawake kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda afya na mazingira.
Hatua hii imepongezwa na washiriki wengi wa kikao hicho, wakieleza kuwa ni mwanzo mzuri wa mabadiliko chanya kwa walimu wanawake, si tu kielimu bali pia kiuchumi na kijamii.