Wanafunzi 21 wa shule ya Msingi Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam wamewasili kwenye mji wa Istanbul nchini Uturuki kwaajili ya ziara ya kimasomo na utalii.
Wanafunzi hao wakiambatana na baadhi ya walimu wa shule hiyo walisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda nchini humo na watakuwa nchini humo kwa siku 10.
Akizungumza siku ya Jumapili Desemba 15, 2024, mkuu wa msafara huo, Goodluck Karashani amesema kuwa wanafunzi hao ni wale walio kwenye chama cha skauti shuleni hapo na kwamba imekuwa utaratibu wa kawaida kwa wanafunzi wa shule hiyo kutembelea nchi mbalimbali kwa lengo la kujifunza mambo mapya ya elimu na masuala ya skauti.
Amesema wanafunzi hao wanapofika katika nchi hizo hujifunza mambo mapya ambayo yanawajenga kiakili na kuwajengea uwezo wa kujiamini kwenye shughuli mbalimbali wanazofanya.
“Umekuwa utaratibu wa kawaida kwa vijana wetu wa skauti kutembelea mataifa mbalimbali kujifunza tamaduni mbalimbali za mataifa mengine, kwa hiyo ziara hii ya kielimu huwa tunaamini kwamba zinasaidia kuwajenga wanafunzi wetu kiakili,” amesema
Amesema ziara za wanafunzi hao katika nchi hizo zimelenga kuwajengea wanafunzi hao uwezo wa kujiamini na kuona mambo mapya kwingine duniani.
“Tusiime ni shule kubwa na mambo yake ni makubwa kama haya ya kupeleka wanafunzi nje ya nchi kwa ziara za mafunzo kila mwaka, siyo jambo dogo, tunaupongeza uongozi wa shule ya Tusiime kwa kuweka kipaumbele masuala ya taaluma na kuwajengea wanafunzi hali ya kujiamini,” amesema na kuongeza,
“Kuwapa wanafunzi fursa kama hizi ndiko kunaifanya shule ya Tusiime kuendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya kitaifa na hata ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, ukiangalia matokeo ya Tusiime kila mwaka yako juu kwasababu ya mambo kama haya”.