Rwanda imewaongoza wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) waliokuwa wakihudumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuondoka eneo la mzozo na kuelekea Tanzania, ikiwa ni sehemu ya hatua ya kuhitimisha operesheni ya kijeshi ya jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, na msemaji wa Jeshi la Rwanda Ronald Rwivanga, vikosi hivyo vilianza rasmi kuondoka siku ya Jumanne, kupitia mpaka wa Gisenyi, Rwanda, wakielekea Tanzania kwa usalama.
Kufikia katikati ya Machi, SADC ilitangaza kuwa itasitisha operesheni ya kikosi chake maalum cha ulinzi kilichopelekwa mashariki mwa Congo, kinachojulikana kama SAMIDRC, na kuanza rasmi zoezi la kuondoa wanajeshi wake.
Kikosi hicho kilichojumuisha wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika Kusini, na mataifa mengine ya kusini mwa Afrika, kilikuwa kikiisaidia serikali ya Kinshasa katika mapambano dhidi ya waasi wa M23, kundi linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda – madai ambayo Kigali imekuwa ikikanusha vikali.
“Uwepo wa vikosi vya SAMIDRC ulikuwa ni suala nyeti katika mzozo huu, na hatua ya kuanza kwa kuondoka kwao ni ishara njema kwa mchakato wa amani unaoendelea,” alisema Nduhungirehe kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).
Msemaji wa Jeshi la Rwanda, Kanali Ronald Rwivanga, alithibitisha kuwa sehemu ya vikosi vya SAMIDRC vilivuka mpaka kupitia Gisenyi, wakisindikizwa na maafisa wa usalama wa Rwanda, na kuingia Tanzania ambapo msafara huo ulitarajiwa kufika baada ya saa chache.
Shahidi mmoja kutoka Gisenyi alisema kuwa msafara wa magari ya kijeshi wapatao 20, ukiwa na wanajeshi wa Tanzania na Afrika Kusini pamoja na vifaa vya kijeshi, ulionekana ukivuka mpaka, ukiwa na ambulensi yenye alama za SAMIDRC.
Chanzo kutoka kundi la M23 kilieleza kuwa ni nusu tu ya vikosi vilivyokuwa katika eneo la Goma ndivyo vilivyoondoka Jumanne, huku nusu nyingine ikitarajiwa kuondoka katika siku chache zijazo.
Licha ya jitihada za kimataifa kupunguza mvutano, mzozo kati ya Congo na Rwanda unaoambatana na masuala ya usalama, mauaji ya kihistoria ya Rwanda, na udhibiti wa rasilimali adimu mashariki mwa Congo, umeendelea kuwa wa muda mrefu na wa gharama kubwa kwa binadamu.
Mashambulizi ya kundi la M23 yamesababisha maelfu ya vifo, huku mamia ya maelfu wakilazimika kuhama makazi yao katika mikoa ya mashariki.
Rwanda imeendelea kukanusha madai ya kuhusika na uungaji mkono wa waasi, ikieleza kuwa wanajeshi wake wanaimarisha ulinzi wa mipaka yake dhidi ya makundi yenye uhasama.
Wakati huohuo, juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Angola na Qatar, pamoja na mazungumzo ya hivi karibuni mjini Washington, zimeanza kutoa matumaini. Congo na Rwanda zilikubaliana kutoa mpango wa amani kufikia Mei 2, 2025.