Wananchi wa kata ya Ivuna Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe wameiomba Kampuni ya Helium One kuwatengenezea barabara ya kutoka Itumbula mpaka Samang’ombe kwa ajili ya kuokoa afya ya mama na mtoto ambao wamekuwa wakipata adha ya usafiri kipindi cha masika wakielekea kujifungua.
Helium One ni kampuni inayotelekeza mradi wa gesi ya Helium katika bonde la ziwa Rukwa ulioanza mwaka 2015, mradi huo una mita za ujazo zipatazo bilioni 138, na kwa sasa upo katika hatua za mwisho kuelekea uzalishaji .
Kuanzia mwaka 2021 mpaka 2025 kampuni ya Helium One imekwisha chimba visima vinne, ambapo mafanikio makubwa yalionekana kwenye kisima cha Itumbula West Well 1 kilichogundulika kuwa na mkusanyiko wa gesi ya helium inayofikia mpaka kiwango cha asilimia 7.9. Utafiti wa kina uliofuata pia ulionesha uwepo wa mkusanyiko wa gesi hiyo katika kisima chake kwa kiwango cha asilimia 5.5 juu ya ardhi.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika kambi ya Itumbula East, Aprili 24, kijijini hapo Mwenyekiti wa kijijini cha Samang’ombe, Chapasi Mpauka amesema shida kubwa iliyopo katika kata ya Ivuna pamoja na vijiji vyake ni ukosefu wa kituo cha afya pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara ambayo imeonekana kuwa changamoto kwa wamama wajawazito wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe, Mjiolojia Chone Malembo, amesema pamoja yakuwa mradi wa gesi ya Helium haujaanza kufanyakazi lakini wananchi wa Itumbula, Ivuna na wilaya nzima ya Momba wameanza kunufaika na mradi huo ikiwemo kulipwa fidia pamoja na kuboreshewa sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu.
“Nimradi ambao umekuwa muhimu natunaimani kuwa utakapoanza kuzalisha na kwasababu bidhaa wanazozizalisha zinatakiwa duniani kote mchango wake kwenye maendeleo ya Itumbula, Kata ya Ivuna pamoja na wilaya ya Momba na nchi kwa ujumla utakuwa ni mkubwa sana ,”
Sambamba na hayo , Malembo amebainisha kuwa, katika mwaka 2023/2024, mkoa ulikusanya zaidi ya shilingi bilioni 37 kutokana na shughuli za madini na kwa robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ulikusanya zaidi ya bilioni 36, na matarajio ni kufikia bilioni 40 ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha.
Balozi wa Gesi ya Helium kutoka Wizara ya Madini, Venosa Ngowi, ameeleza kuwa Tanzania ina akiba ya zaidi ya futi bilioni 138 za ujazo wa gesi ya helium, jambo linaloiweka nchi kwenye ramani ya dunia kama mmoja wa wazalishaji wakubwa wa gesi hiyo.
Ngowi amefafanua kuwa, gesi hiyo ina matumizi muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya (hasa kwenye MRI Scanner), teknolojia ya anga, utafiti wa sayansi ya angahewa, pamoja na usafiri wa anga kama vile roketi na vifaa vya ndege.