Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma Shaban Millao, amesema maandalizi yote ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamekamilika na kuwaomba wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumatano, Novemba 27, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kijijini Bukulu, Millao ameeleza kuwa vifaa vyote muhimu kwa ajili ya uchaguzi vimepatikana na mipango ya kufanikisha zoezi hilo imekamilika kikamilifu.
Kwa mujibu wa Millao, wapiga kura 124,129 wamejiandikisha katika Halmashauri ya Kondoa, ambapo wanaume ni 64,018 na wanawake ni 60,111, sawa na asilimia 96 ya malengo ya usajili. Katika uchaguzi huo, jumla ya nafasi 2,100 za uongozi zinagombewa, ikiwa ni pamoja na nafasi za wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa halmashauri za vijiji kutoka makundi ya mchanganyiko na wanawake, pamoja na wenyeviti wa vitongoji. Vyama vya siasa vimeonesha hamasa kubwa kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni na maandalizi ya uchaguzi.
“Halmashauri yetu tangu tuanze zoezi hili tumekua na mahusiano mazuri na Viongozi wa Vyama vya Siasa, tukijitahidi kuhakikisha nia ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, uchaguzi wetu unafanyika kwa amani na utulivu tukishirikiana vyema na vyama hivi katika hatua zote muhimu”, amesema Millao.
Uchaguzi huo utafanyika katika vituo vilivyotumika wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. Millao amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuhakikisha viongozi wanaopatikana ni wale wanaowakilisha matakwa ya wananchi, na akasisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi.