Latest Posts

WANANCHI WALIA NA UBOVU WA BARABARA, TARURA YAAHIDI KUSHUGHULIKIA

Na Helena Magabe – Tarime

Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, baadhi ya maeneo kwenye barabara za Tarime Mjini pamoja na vijijini zimeharibika kiasi kwamba nyingine zinapitika kwa taabu sana na nyingine vyombo vya moto vinakwama kabisa. Wananchi wameiomba TARURA kutatua changamoto hizo za barabara ambazo zimekuwa kero kubwa msimu wa mvua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watumiaji wa barabara inayoanzia Kata ya Nkende, inapita Kata ya Nyandoto na kuunganisha Kata za Mwema na Susuni (Tarime Vijijini), wameelezea maeneo yanayowapa shida msimu huu wa mvua, wakiiomba TARURA kutoa msaada wa haraka.

Benadeta Marwa, mtumiaji wa barabara hiyo, alitaja maeneo kama Kinyambi, Kanda Maalum, Nyagisese pamoja na Kambi ya Jeshi la JWTZ – yote yakiwa ndani ya Kata ya Nyandoto, Tarime Mjini. Alisema kuwa licha ya kulipa ushuru kutokana na shughuli zake za biashara, barabara zikiharibika huchukua muda mrefu kutengenezwa. Aliongeza kuwa TARURA ilibuni njia mbadala, lakini nayo ina changamoto zake.

Cheina Weisiko (Mchina) pamoja na Mwita Marwa wamelalamikia ubovu wa vipande mbalimbali vya barabara hiyo yenye watumiaji wengi, wakiomba TARURA ichukue hatua za haraka kuwasaidia wananchi wanaolipa kodi lakini hupata adha kubwa wakati wa mvua.

Mjasiriamali Daniel Ngerecha Mniko (Surambili), muuzaji wa nguo za mitumba aliyekuwa akielekea mnadani kwa kitenga, alisema alikwama barabarani kwa zaidi ya saa moja na kuiomba serikali ichukue hatua za haraka kutengeneza maeneo hayo.

Mwandishi wa Jambo TV alitembelea maeneo hayo Aprili 22, 2025, na kushuhudia magari yakiwa yamekwama pande zote mbili za barabara kwa zaidi ya saa moja. Dereva mmoja wa roli alilazimika kushusha tofali barabarani ili kupunguza uzito. Aidha, alishuhudia boda boda ikianguka na kujaa tope.

Mbali na hayo, wananchi wa Kata ya Nkende wamelalamikia pia ubovu wa barabara inayokwenda uwanja wa ndege, inayopita shuleni hadi kituo cha afya Nkende. Wamedai kuwa hata barabara mbadala iliyolimwa na TARURA nayo haipitiki kwa sababu haina makaravati wala mitaro.

Nyamaisa Masero Keraryo (mkazi wa Seng’ensa), Baraka Mwita Mkono (mkazi wa Kogesenda) pamoja na Kizani Obwige, walieleza kuwa ubovu huo umesababisha magari ya watalii yanayoingia na kutoka uwanja wa ndege kulazimika kuzunguka kupitia Kata ya Regicheri, Tarime Vijijini. Obwige aliongeza kuwa kipande kinachosababisha usumbufu ni cha mita chache tu ambacho hakipaswi kuchukua muda kurekebishwa.

Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Mji Tarime na Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Tarime, Bashiri Abdalla Suleiman, alishauri Halmashauri itengeneze barabara ya kuingia uwanja wa ndege bila kutegemea TARURA. Alisema kuwa Halmashauri hupokea shilingi milioni 20 kila mwezi, kwaajili ya uwanja wa ndege ikilinganishwa na milioni 11 zilizokuwa zikipokelewa mwaka 2020 alipokuwa Makamu Mwenyekiti. Alitoa rai Halmashauri kutumia mapato hayo kutengeneza barabara hiyo.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Tarime, Charles Marwa, Aprili 23, 2025, alikiri kuwepo kwa changamoto hizo. Alisema baadhi ya vipande vimekuwa vikishughulikiwa mara kadhaa kwa changarawe, lakini mvua inaponyesha, tatizo hurudi. Alifafanua kuwa wametenga bajeti ya dharura ya zaidi ya milioni 100 kupitia fedha za TACTIC kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya maeneo korofi zaidi.

Alieleza kuwa barabara ya Nkende–Butobori ina vipande vyenye changamoto kubwa, hasa kutokana na matumizi ya maroli makubwa yanayobeba mirunda na mchanga. Alisema maroli yanaruhusiwa kubeba chini ya tani 10, lakini wengi huzidisha ,na adhabu ya kubeba zaidi tani 10 faini ni zaidi ya milioni 7.

Aliongeza kuwa kipande kilicho korofi zaidi kiliharibika baada ya roli lililobeba mirunda kukwama na kutengeneza shimo. Alisisitiza kuwa eneo hilo linahitaji bajeti kubwa kujengewa mitaro na makaravati imara. Barabara ya Nyagisese kwenye nyumba za Kanda Maalum nayo inahitaji kujazwa kifusi ili kuinuliwa – bila hivyo, hata karavati likiwekwa ni KAZI Bure.

Aidha, barabara ya Rebu Senta – Kibaga Mine imeanza kufanyiwa kazi na mkandarasi. Hali kadhalika, kuanzia jana mkandarasi ataendelea kurekebisha vipande korofi kwenye barabara ya Nkende–Butobori. Barabara ya kuelekea uwanja wa ndege itafungwa kwa kuwa inapita katikati ya Shule ya Sekondari Magena, kati ya madarasa na vyoo, ambapo wazazi waliomba ifungwe. Mchakato unaendelea, na watumiaji watalazimika kutumia barabara ya kupitia Kata ya Regicheri, Tarime Vijijini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!