Latest Posts

WANATEMEKE KUPATA HUDUMA YA KARIBU YA USAFISHAJI DAMU KWA WENYE CHANGAMOTO YA FIGO

Na Didas Olang, Dar es Salaam.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke (TRRH) rasmi imeanza kutoa huduma ya kusafisha Damu kwa wagonjwa wenye changamoto za figo (Dialysis) Juni 14, 2024 ambapo mgonjwa mmoja amepatiwa huduma hiyo hospitalini hapo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Daktari Joseph Gaspar Kimaro amesema hospitali imekiwezesha kitengo chake cha usafishaji damu kwa kufanya ununuzi wa mashine kumi za kusafisha damu pamoja na vifaa vyake vyenye uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wawili kwa siku kwa kila kifaa kimoja na kuweka uwiano wa kuwahudumia jumla ya wagonjwa takribani 20 kwa siku.

“kwa wakati mmoja tuna uwezo wa kuwahudumia wagonjwa kumi, na session moja inadumu kwa wastani wa saa tatu hadi nne, maana yake angalau wagonjwa wawili hadi watatu kwa kila mashine” Amesema Dkt. Kimaro.

Amesema ununuzi wa mashine hiyo umegharimu Shilingi za Kitanzania milioni 400 ya mapato ya ndani ya Hospitali

“Hii ni heshima kubwa kwa Serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Daktari Samia Suluhu Hassan, inayotoa miongozo ya kututaka kutenga sehemu ya mapato yetu ya ndani ili kuboresha huduma kwa wananchi” Ameeleza Dkt. Kimaro.

Dkt. Kimaro ameongeza kuwa kuanzishwa kwa huduma hiyo hospitalini hapo kumelenga kupanua wigo wa huduma karibu na wananchi pamoja na kupunguza Rufaa za huduma ya kusafisha damu kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo kwa mwaka walikuwa wakitoa rufani zaidi ya 200 za wagonjwa wenye matatizo ya figo.

Aidha Dkt Kimaro ametoa rai kwa jamii kuendelea na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yanayochangia pakubwa changamoto ya figo kwa kufanya mazoezi na kufuata ushauri wa madaktari kwenye matumizi ya dawa.

Kwa niaba ya Timu ya wataalamu wa huduma ya kusafisha damu, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani Farida Mtonga, amesema wamepokea mafunzo elekezi ya namna bora ya kutumia mashine hiyo kwa ufanisi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  na kuahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Kwa upande wake mzazi wa mgonjwa wa kwanza aliyepatiwa huduma ya kusafisha damu, Humphrey Thadei Tarimo ameishukuru Serikali kupitia hospitali ya Rufaa ya Temeke kuwasogezea huduma hiyo karibu na kuwaepusha na msongamano mkubwa wa kupata huduma hiyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuiomba kuwafanyia unafuu katika zoezi la upandikizaji figo kwa mgonjwa wao kwani mtu wa kujitolea figo amekwishapatikana.

“Huyu binti bado umri wake ni mdogo (mgonjwa) kufanyiwa dialysis kwa maisha yake yote itakuwa ni ngumu, tunaiomba serikali iweze kutuangalia kwa jicho la tatu kwa sababu tumeshapata mtu wa kuchangia figo basi itufanyie unafuu ili tuweze kumpandikiza figo aendelee na maisha ya kawaida kama wengine” Ameeleza Dkt. Kimaro.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!