Wakazi wa vijiji mbalimbali katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, wamepewa elimu kuhusu tafsiri ya sheria ya umiliki wa ardhi, haki zao za kimiliki, matumizi ya ardhi, na wajibu wao katika usimamizi wa ardhi.
Elimu hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na wataalamu wa sheria na ardhi kutoka timu ya kampeni ya Msaada wa Sheria wa Mama Samia, waliotembelea vijiji hivyo kwa ajili ya kutoa elimu na msaada wa kisheria.
Miongoni mwa masuala yaliyotolewa ufafanuzi ni namna ya kutwaa ardhi, hoja iliyoulizwa na wanakijiji wa Mloka na kujibiwa na Mratibu wa kampeni hiyo katika wilaya hiyo, Wakili Gloria Baltazari kutoka Wizara ya Katiba na Sheria.
Hoja nyingine ilihusu haki ya mmiliki wa ardhi iwapo madini yanagunduliwa kwenye eneo lake, swali lililoulizwa na mwanakijiji wa Mohoro na kujibiwa na Afisa Ardhi wa timu hiyo, Bw. Zephania Sabo.