Wanawake wameombwa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima ili waweze kuepukana na mikopo ambayo inawaumiza na kuwapelekea kutofikia malengo.
Hayo yameelezwa na Mchumi kutoka Kitengo cha Mipango na Uratibu Mkoa wa Mtwara, Lucy Kikweve wakati wa kilele cha Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani Machi 8,2025 yaliyofanyika kimkoa Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Ambapo Kitweve amesema ni muhimu kila unapoweka mipango yako kujitathimini na kujua kama upo ndani ya bajeti ya kile unachokiingiza kwani matumizi hayapaswi kuwa makubwa kuliko kiasi unachokiingiza.
Sambamba na hilo amewataka wazazi kuwapa watoto elimu hususani wanawake ili waweze kujisimamia kwenye maisha kwani kupitia elimu kutamuwezesha mwanamke kujisimamia mwenyewe.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amesema katika sekta mbalimbali zilizopo hapa nchini wanawake wanaongoza katika shughuli za uzalishaji.
Aidha ametoa rai kwa wazazi na wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano katika shughuli zote za maendeleo ya kielimu katika maeneo yanayowazunguka ili kupata maendeleo tarajiwa kwa wakati sahihi ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu ya shule,wazazi kuwapeleka watoto shule,kuchangia chakula cha watoto wanapokuwa shuleni.
Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa wanawake na wasichana (UN WOMEN) Pelagia Kijuu, amesema Shirika hilo limefanikiwa kutoa uhamasishaji na uelewa kuhusiana na haki ya wanawake kushiriki nafasi mbalimbali za uongozi ambapo mwaka 2024 wanawake wengi wamejitokeza kuchukua fomu na kufanikiwa kupata nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na takwimu za mwaka 2019.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wilaya ya Mtwara mjini UWT Victoria Tungu amesema chama hicho kinatambua na kuthamini wanawake hivyo amewataka wanawake kutokata tamaa kwenye kuwania nafasi mbalimbali za uongozi hasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ambao unawahusisha madiwani na wabunge.
Maadhimisho hayo ya siku ya wanawake mwaka 2025 yanaenda na kauli mbiu inayosema ‘Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji