Watumishi wa afya wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma General wamesisitizwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi ili kujenga imani kwa wateja wao.
Msisitizo huo umetolewa Ijumaa Septemba 20,2024 hospitalini hapo na Afisa Afya Mkoa wa Dodoma Nelson Rumbeli wakati akitoa mafunzo kwa watumishi hao namna ya utekelezaji wa mkakati wa ‘Spot Check’.
Rumbeli amesema serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa hivyo kama wataalam na watoa huduma ni wajibu sasa kuhakikisha huduma zinakuwa bora ili kupunguza vifo vinavyoweza kujitokeza kwa uzembe.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi hao namna ya kutekeleza mkakati wa ‘Spot check’ ambao unatekelezwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa madhumuni ya kuboresha huduma za afya nchini.
‘’Spot Check’ ni mkakati mzuri sana ambao unatusaidia kuanisha changamoto katika kipindi kifupi lakini pia kuzipatia ufumbuzi wa haraka ili kuboresha huduma,’’
‘’Mkakati huu unatekelezwa katika nyakati tofautitofauti, tunafahamu kwamba ipo mikakati mbalimbali ambayo serikali imefanya , nipo mikakati shirikishi ipo, mikakati ya kifedha, na mfano Waziri wa Tamisemi, na Rais wa Samia wamekuwa wakizungumzia sana suala hili la ubora wa huduma hivyo watumishi wenzangu tuwajibike isavyo,’’ Amesema Rumbeli.