Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa TAWA linamshikilia Riziki Charles Mapila (55) mkazi wa Lubele Wilaya ya Kyela mkoani humo akiwa na nyara za Serikali vipande tisa vya meno ya Tembo bila kibali.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema mtuhumiwa alikamatwa mnamo aprili 14, 2025 na Askari waliokuwa doria katika Kitongoji cha Isaki Kata ya Njisi, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela akiwa na vipande 9 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilogram 34.6 ambavyo alikuwa amevihifadhi ndani ya mfuko wa sandarusi kisha kuficha porini.
Amesema wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na askari wa TAWA Wilayani Mbarali, linamshikilia Kenedy Yawaga (37) Mkazi wa Itamba Mbarali akiwa na nyara za Serikali vipande vitatu vya meno ya Tembo bila kibali.
Polisi kupitia kamanda wake mkoani Mbeya inasema mtuhumiwa alikamatwa Aprili 03, 2025 katika Kijiji cha Mabadaga Kata ya Mapogoro, Tarafa ya Rujewa, Wilayani Mbarali katika operesheni maalum dhidi ya wahujumu Uchumi wa Taifa akiwa na nyara hizo zenye uzito wa kilogram 12 naye akiwa amefunga kwenye mfuko wa sandarusi na kisha kufukia ardhini kwenye shamba lake lililopo kwenye mji wake.
Kamanda Benjamin Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa walikuwa wanajihusisha na uwindaji haramu katika hifadhi za Taifa na kwamba taratibu za kuwafikisha Mahakamani zinaendelea.