Latest Posts

WAZAZI/WALEZI WAMETAKIWA KUSIMAMIA MIENENDO YA WATOTO

Wazazi na walezi wametakiwa kuwasimamia ipasavyo wanafunzi wanapokuwa nyumbani ili kuepuka kuwa na matokeo mabaya shuleni.

Hayo ameyazungumza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Likombe Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara Mwinyi Mzaina wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mashine ya kudurufia mitihani (photocopy machine) kwenye shule ya mfano ya sekondari ya Likombe iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Mzaina amesema wapo wazazi ambao wanashindwa kuwajibika kikamilifu kwa watoto hali inayopelekea baadhi ya watoto hao kuonekana kwenye matukio yasiyokuwa rafiki kwao.

Mashine hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga iliyogharimu shilingi milioni 2.8. lengo likiwa ni kuwapunguzia adha wazazi ya kuchangia shilingi elfu 3,500 kila mmoja wao fedha kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji na mashine hiyo.

“Ili elimu iwe sawasawa lazima watu wanne wawajibike vizuri ambao ni serikali kuwajibika kwenye kutengeneza miundombinu rafiki kwa wanafunzi, wazazi kuandaa na kufanya maandalizi ya kuwapeleka shule, walimu wawajibike kuzingatia vipindi na kufundisha kwa wakati na jukumu la mwanafunzi kuhakikisha anataka kusoma”amesisitiza Mzaina

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, amewaomba wazazi kujizatiti katika kuwahamasisha watoto waweke elimu kuwa kipaumbele chao ili waweze kujikwamua kwenye maisha yao ya baadae.

Mkuu wa shule hiyo, Hadija Mkambala amesema ukosefu wa mashine hiyo ni miongoni mwa changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili ambapo ilikuwa inawalazimu kwenda kudurufia mitihani shule jirani hali iliyopelekea kutokuwa na mitihani ya kujipima hivyo ufaulu kuwa wa chini kwa wanafunzi.

Katika hatua nyingine Mtenga ameendelea kukabidhi vifaa mbalimbali vya ujenzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo bati, tofari na saruji kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya mama lishe waliyopo Nkanaredi na kwa bodaboda kwa ajili ya kujenga sehemu za kujikinga na jua na mvua kijiwe cha Rehemani Mikindani kwenye halmashauri hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!