Wazazi na walezi wamehaswa kuwajengea watoto misingi bora ili waje kuwa viongozi wenye maadili ambao watakuwa watenda haki na kuliepusha taifa kuwa na vijana wasiokuwa na maadili.
Hayo ameyazungumza Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii Taifa Bakwata Hawa Abderehman Ghasia wakati wa Fainali ya mashindano ya kuhifadhi Quraan tukufu yaliyofanyika katika Kijiji na kata ya Naumbu Halmashauri ya wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara.
Hivyo kupitia mashindano hayo Hawa Ghasia amewaomba wazazi kutodharau elimu ya dini kwani kupitia elimu hiyo itasaidia kujenga viongozi wenye hofu ya Mungu,wenye maadili.
“Ili kuisaidia chi yetu lazima hawa watoto tuwajenge kimaadili tuwaandae waje kuwa watumishi wazuri wa serikali na viongozi wazuri sana ambao wanaweza kutenda haki kwasababu watakuwa wanamuogopa Mungu.”Amesema Ghasia
Pia amewataka wazazi kujitahidi kuwasaidia walimu wa madrasa kwakutoa michango ili iweze kuwasaidia walimu hao pamoja na kuwasaidia kwenye shughuli zao binafsi kama vile kuwalimia kwenye mashamba yao ili kuwapa motisha ukizingatia hawana mshahara.
Nae Katibu wa Bakwata mkoa wa Mtwara Mussa Saidi amewaomba walimu wa madrasa wajitahidi kuendana na mitaala ya serikali na amewataka vijana hao ambao wameshiriki kwenye mashindano hayo ya kuhifadhi Quraan tukufu kutumia elimu waliyopata kwa kufanya vitu vyenye manufaa kwa jamii zao pamoja na kuusogeza mbele Uislamu.
“Waislamu tunatakiwa tujitathimini kama tunapatia au laa,twende tufanye mambo yanayoendana na serikali inavyotaka tunazo madrasa lakini pia tunatakiwa madarasa hizo tufuate mitaala ya serikali tusije tukaachwa nyuma,tukiweza tufikie mahala kama tuna watoto wakubwa kwenye madrasa zetu tuweke cherehani ili mtoto akitoka hapo anajua hata kushona sio vibaya.”
Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Jamaldin Salim amewataka walimu kuweka ratiba nzuri ambayo itaendelea kuwasaidia wanafunzi hao kupata elimu ya dini kutokana na kuingiliana na ratiba ya elimu ya kawaida na amewasisitiza wazazi kushirikiana na walimu kuwahimiza watoto kusoma elimu ya dini.
Sambamba na hilo Hawa Ghasia ametoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa mashindano hayo ya kusoma Quruan kuanzia juzuu 1 hadi juzuu 7 ambapo washindi wamefanikiwa kupata zawadi kama vile TV kuanzia nchi 32 had 65,pasi na feni.