Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amekipongeza kiwanda cha kutengeneza maji tiba cha Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited kilichoko mkoa wa Pwani.
Ametoa pongezi hizo siku ya Alhamisi Februari 20, 2025 alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujionea uzalishaji wa maji tiba na kuzungumza na mwekezaji wa kiwanda hicho.
Waziri Mhagama amesema amefurahi kufanya ziara katika kiwanda hicho ambapo ameona namna uzalishaji maji tiba unaotumia teknolojia ya kisasa unavyofanyika, akitanabaisha kuwa serikali inajivunia uwekezaji unaofanywa na taasisi binafsi ikiwemo Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited.
Amesema utengenezaji wa maji tiba hayo nchini unapunguza gharama za usafirishaji pamoja na kupunguza muda wa kusubiri dawa kutoka nje ya nchi. Aidha amesema uwekezaji uliofanywa na Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited, unaipa faraja na nafuu serikali kwani inasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza maji tiba hayo.
Waziri Mhagama ameahidi kuwa serikali chini ya Wizara yake itaendelea kutatua changamoto zinazoikabili sekta binafsi kwani sekta hiyo ndiyo mdau mkubwa wa serikali katika maendeleo nchini.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kutafuta masoko nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Waziri ameiomba Bohari ya Dawa (MSD) ambayo ina dhamana ya kusambaza dawa ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupeleka dawa zinazotengenezwa na wazawa ikiwemo zinazozalishwa na Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited.
Naye Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Dkt. Muganyizi Kairuki ameishukuru serikali kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta binafsi na kuiomba kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ambazo zinasababisha kudorora kwa uzalishaji.
Katika ziara hiyo, Waziri Mhagama aliongozana na viongozi mbalimbali kutoka taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Pwani