Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, leo Machi 03, 2025 amezindua rasmi mfumo mpya wa kidijitali wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) unaojulikana kama NBC Kiganjani. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa The SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa na viongozi wa serikali, sekta ya fedha, wadau wa biashara na maendeleo pamoja na wananchi.
Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu ameipongeza benki ya NBC kwa kuwa benki inayoongoza katika uvumbuzi wa teknolojia za kifedha nchini.
Amesema kuwa huduma hiyo ni hatua kubwa katika kuimarisha uchumi wa kidijitali, ikiendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia, kupitia salamu zilizowasilishwa na Waziri Mkuu, ameipongeza NBC kwa mageuzi hayo, akisema kuwa huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kujenga uchumi imara wa kidijitali. Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, naye amepongeza NBC kwa hatua hiyo, akisema benki hiyo imekuwa kimbilio la Watanzania wengi kwa huduma zake bora na za kuaminika.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amepongeza NBC kwa kuanzisha mfumo huo wa kidijitali, akisema kuwa utaongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania wengi zaidi.
Amebainisha kuwa NBC Kiganjani ni jukwaa litakalorahisisha huduma za benki kwa wateja wa aina zote, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa turufu muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Aidha, ameipongeza NBC kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya michezo kwa kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kuifanya kuwa moja ya ligi bora barani Afrika.
Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anayesimamia uthabiti wa sekta ya fedha, Sauda Msemo, amewakumbusha wananchi kuhakikisha wanapata huduma za kifedha kupitia taasisi zilizosajiliwa rasmi ili kuepuka utapeli.
Amesema kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga la UVIKO-19 mwaka 2019, sekta ya fedha imeendelea kuimarika, huku mikopo chechefu ikipungua hadi asilimia 3.43 kutoka zaidi ya asilimia 10 miaka mitano iliyopita.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, amesema kuwa, huduma mpya zinazozinduliwa ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kifedha unarahisishwa kwa wateja wa aina zote. Huduma hizo ni pamoja na NBC Kiganjani, ambayo ni aplikesheni ya kidijitali inayomwezesha mteja kufungua akaunti, kuhamisha fedha, kulipa bili, kupata mikopo na kufanya miamala mingine bila kutembelea tawi la benki. Pia, imezinduliwa NBC Lipa Kiganjani, inayowezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kufanya malipo kwa kutumia simu za mkononi badala ya mashine za POS.
Huduma nyingine mpya ni NBC Education Connect, mfumo wa malipo ya ada za shule kwa njia rahisi na salama, ukiwawezesha wazazi na taasisi za elimu kufanya malipo bila usumbufu.
Aidha, benki hiyo imeanzisha huduma ya mikopo ya Salary Advance kupitia NBC Kiganjani, ambapo mteja anaweza kupata mkopo ndani ya dakika moja kupitia aplikesheni hiyo.
Sabi ameongeza kuwa mfumo huu umetengenezwa na vijana wa Kitanzania, hatua iliyoiwezesha benki kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 3 ambazo zingetumika kwa huduma za wataalamu wa nje.
Amebainisha kuwa NBC Kiganjani imeundwa mahsusi kwa ajili ya Watanzania, ikihakikisha urahisi wa huduma na usalama kwa kutumia teknolojia kama utambuzi wa sura, alama za vidole na One Time Password (OTP).
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa serikali inaunga mkono juhudi za maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa kidijitali.
Amesema mazingira mazuri ya kibiashara yanayowekwa na serikali yamewezesha benki kama NBC kuendelea kuimarika, huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kubuni mifumo inayorahisisha huduma kwa wananchi.
Uzinduzi wa NBC Kiganjani ni hatua kubwa katika mageuzi ya kidijitali ndani ya sekta ya fedha nchini, huku ukitarajiwa kuwanufaisha maelfu ya Watanzania kwa urahisi wa huduma, usalama na gharama nafuu.