Latest Posts

WAZIRI ULEGA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA MIRADI YA BRT, AAGIZA IKAMILIKE KABLA YA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA

 

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kushtukiza kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) usiku wa kuamkia leo Jumamosi tarehe 28 Desemba, 2024 jijini Dar es Salaam
Meneja wa Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Mhandisi Allen Natai (kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega (katikati) wakati wa ziara ya Waziri huyo usiku wa kuamkia leo Jumamosi tarehe 28 Desemba, 2024 kwenye miradi ya BRT kuona mwenendo wa utekelezaji wake ikiwemo agizo la kufanya kazi usiku na mchana.
Kulia kwa Waziri Ulega, ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta.

Kazi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) zikiwa zinaendelea usiku katika mradi wa BRT 4 katika baraba ya Mwenge hadi Tegeta kama zilivyokutwa na mpiga picha wetu usiku wa kuamkia leo Jumamosi tarehe 28 Desemba, 2024 wakati wa ziara ya kushtukiza ya Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega.

Matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega usiku wa kuamkia leo Jumamosi tarehe 28 Desemba, 2024 katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kushtukiza usiku wa kuamkia leo Jumamosi tarehe 28, Disemba 2024 yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Waziri Ulega ameagiza miradi hiyo ikamilike kabla ya msimu wa mvua za Masika mapema mwakani ili kupunguza changamoto za msongamano wa magari katika jiji hilo.

“Nimeagiza kazi ifanyike usiku na mchana kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati. Msimu wa Masika una changamoto zake, na hatutaki kuona wananchi wakitaabika. Tunafanya hivi kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais pamoja na Ilani ya CCM ya 2020-2025 inayosisitiza kupunguza msongamano wa magari mijini,” amesema Waziri Ulega.

Katika ziara yake hiyo , Waziri Ulega alikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya BRT 1 kutoka Ubungo hadi Kimara pamoja na barabara ya Mwenge kuelekea Tegeta inayojumuishwa katika mradi wa BRT 4.

Amesema, ameridhishwa na kasi ya kazi zinazofanywa na wakandarasi ambao wameanza kutekeleza agizo lake la kufanya kazi saa 24 kwa siku.

“Timu ya usimamizi ya TANROADS chini ya Mtendaji Mkuu wake, Mhandisi Mohamed Besta, inafanya kazi nzuri. Wakandarasi lazima wafanye kazi muda wote bila kupoteza muda. Watanzania wanatamani kuona miradi hii ikikamilika, na sisi kama serikali tunajali maslahi yao,” ameongeza Waziri Ulega.

Kwa upande wake, Mhandisi Mohamed Besta amemhakikishia Waziri kuwa TANROADS itaendelea kusimamia wakandarasi kwa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

“Tutaendelea kufanya hivi (kusimamia wakandarasi kufanya kazi usiku na mchana) Hata pale ambapo Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi hautakuja kufanya ziara za kushtukiza, tutahakikisha kazi inaendelea kwa kasi ili kufanikisha lengo la kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema Mhandisi Besta.

Naye Meneja wa Mradi wa BRT, Mhandisi Allen Natai, ameeleza kuwa kazi ya kujenga miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka inaendelea vizuri.

Ziara ya Waziri Ulega imeonesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuboresha huduma kwa wananchi na pia imetoa msukumo mpya kwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!