Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama ametoa maelekezo kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kuhakikisha huduma za uzazi wa dharura kwa kina mama zinapatikana ikiwemo vitanda maalum vya kujifungulia na kuwapunguzia adha wananchi ya kufuata huduma za afya maeneo ya mbali.
Waziri Mhagama ametoa maelekezo hayo Oktoba 4, 2024 akiwa katika ziara ya siku Sita Mkoani Kilimanjaro yenye lengo la kukagua na kuzindua miradi ya Sekta mbalimbali iliyotolewa fedha na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo Sekta ya Afya.
Amesema kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 10 ili kutekeleza miradi ya Afya na kwamba Serikali imeongeza milioni 150 kwa ajili ya vifaa tiba vitakavyotumika katika kituo cha Afya Masama Kati.
Waziri Mhagama ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa kukamilisha ununuzi wa vifaa tiba ili Zahanati ya Kimashuku ianze kufanya kazi ifikapo Oktoba 30 mwaka huu.
“Tunatamani Zahanati hii iwe mkombozi kwa akina mama, wazee, vijana na watoto wetu, nitoe wito kwa Halmashauri yetu kuhakikisha Zahanati yetu inasimamiwa vizuri na tunaamini Zahanati hii itaenda kutoa huduma zinazotakiwa kwa kuwa Mhe. Rais Samia ameleta Milioni 100 ya umaliziaji wa Zahanati hii na Milioni 50 ya ununuzi wa vifaa tiba, jambo la kwanza naomba fedha ya vifaa ipelekwe Bohari ya Dawa haraka sana, nataka kuona Zahanati hii upatikanaji wa dawa usiwe wa mashaka.” Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ameshukuru Serikali kwa kutekeleza miradi hiyo muhimu kwa Wananchi wa Jimbo la Hai ikiwemo miradi ya afya,elimu na barabara hali itakayo chochea ukuwaji wa uchumi.
Aidha amewataka Wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi pamoja na kupiga kura ili kupata viongozi wenye sifa.
Miradi iliyo tembelewa na Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama ni pamoja na Shule ya Sekondari Harambee,Kituo cha Afya Masama Kati, Kituo cha Afya Longoi na Zahanati ya Kimashuku.