Latest Posts

WAZIRI WA SHERIA DRC KWENYE KIKAANGO CHA UFISADI: AZIMIO LA UCHUNGUZI LAPITA

Bunge la Taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limepitisha kwa kauli moja azimio la kumruhusu Mwendesha Mashtaka Mkuu kuanzisha uchunguzi rasmi dhidi ya Waziri wa Sheria, Constant Mutamba, anayekabiliwa na tuhuma za kutumia vibaya takriban dola milioni 20 kutoka kwenye mfuko wa fidia kwa waathirika wa vita.

Mutamba, mwenye umri wa miaka 37 na aliyeteuliwa kuwa waziri Mei 2024, ni maarufu kwa kauli zake kali dhidi ya ufisadi, ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya adhabu ya kifo kwa wanaofuja mali za umma. Hata hivyo, sasa yeye mwenyewe anakabiliwa na tuhuma nzito zinazohusisha utoaji wa zabuni yenye thamani ya dola milioni 40 kwa kampuni ya Zion Construction SARL – kampuni ambayo ilianzishwa Machi 2024 na inadaiwa haina uwezo wala watalaamu wa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa gereza karibu na Kisangani.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamati maalum ya Bunge, Mutamba alitoa karibu nusu ya bajeti ya mradi huo – sawa na dola milioni 20 – bila idhini ya Waziri Mkuu, huku fedha hizo zikitolewa kutoka kwenye mfuko wa fidia uliolipwa na Uganda kwa waathirika wa vita vya mwaka 2000.

Katika video ya TikTok iliyosambaa Jumatatu, Mutamba alimshambulia Mwendesha Mashtaka Mkuu, Firmin Mvonde, kwa kumtuhumu kuwa sehemu ya “mafia” inayolenga kumchafua kisiasa. Alidai pia kuwa anatuhumiwa kwa sababu ya msimamo wake dhidi ya rais wa zamani Joseph Kabila, ambaye naye anakabiliwa na tuhuma nzito za kushirikiana na waasi wa M23.

Mutamba amekiri kuwepo kwa “makosa ya kiutawala” kwenye mchakato wa zabuni hiyo lakini amekana kufaidika binafsi, akisema tuhuma zote ni sehemu ya “kampeni ya propaganda ya kupotosha.”

Spika wa Bunge, Vital Kamerhe, kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya taifa, alitangaza uamuzi huo wa kuruhusu uchunguzi, akieleza kuwa: “Bunge limeridhia kwa kauli moja azimio la kuruhusu uchunguzi dhidi ya Mheshimiwa Constant Mutamba.”

Uamuzi huu hauondoi moja kwa moja kinga ya ubunge kwa Mutamba. Endapo uchunguzi utabaini ushahidi wa kutosha, Bunge litalazimika kupiga kura nyingine ili kuondoa kinga hiyo rasmi na kufungua mlango wa kufikishwa mahakamani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!