Wenyeviti wa Vijiji vinavyozunguka pori la akiba Grumeti upande wa Wilaya ya Bunda Mkoani Mara wameliomba Shirika la Grumeti Fund kuwawekea uzio wa umeme kutenga eneo lililohifadhiwa na maeneo ya wananchi ili kuzuia kadhia ya mauaji ya watu na mifugo pamoja na uharibifu wa mazao ambao umekuwa ukifanywa na Wanyamapori wakali na waharibu kwenye Maeneo yao.
Kauli hiyo wameitoa mara baada ya kutembelea kujionea mafanikio baada ya uwepo wa uzio katika Vijiji vya Bonchugu,kazi,Rwamchanga,niseke na Parknyigoti ambapo maeneo hayo yameondokana na uvamizi unaofanywawa na wanayampori baada ya uwepo wa uzio uliowekwa na Shirika la Grumeti fund kwa kushirikiana na Serikali.
“Naenda kufanya Kikao na wananchi Wangu kulikuwa na upotoshaji mkubwa juu ya huu uzio kwamba unapiga shoti watoto, Ni uongo mkubwa, tumezungumza na baadhi ya wananchi ambao wao huku Serengeti wamewekewa na mambo yao yako vizuri, wanalima tumeiona hadi miwa ambayo ni asali kwa tembo Ipo kando ya Hifadhi haijaliwa sababu ya uzio huu. Pia watoto wanakwenda shule bila kuhofia kukutana na tembo wala simba. Aliongeza kusema tunaiomba Serikali iruhusu hili jambo lifanyike kwetu pia maana tunateseka mno”Alisema Ezekiel kahabi mwenyekiti Mtaa wa mashujaa Bunda.
Wenyeviti hao wameenda mbali na kusema kuwa kama uzio utawekwa kwa upande wa Bunda ambako haujawekwa bado utasaidia kuiondolea mzigo Serikali wa kulipa kifuta machozi ambacho hutolewa kila mara kwa wananchi wanaovamiwa na Wanyamapori. Walisema pia kuwa kifuta machozi na kifuta jasho hicho ni kidogo sana kiasi cha kutokidhi mahitaji yao ukilinganisha na mazao yanayoharibiwa na tembo au mali zao zinapouwawa na simba.