Latest Posts

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA MAFUNZO YA UTAWALA BORA WILAYANI RORYA

Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha mafunzo ya utawala bora na uraia kwa kamati za usalama za wilaya, wakuu wa idara za halmashauri, na watendaji wa kata wilayani Rorya, mkoani Mara. Mafunzo haya yanalenga kuwakumbusha viongozi hao kuzingatia mipaka katika utumishi wao na kufuata misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na demokrasia.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Joyce Mushi, ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo, ameeleza kuwa mpango huu ni mwendelezo wa mafunzo yaliyotangulia kufanyika mkoani Rukwa.

Mushi amesema mafunzo hayo yanawalenga kamati za usalama, watendaji wa kata, na watumishi wa idara mbalimbali za halmashauri ili kuwajengea uwezo na kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Rebuilding. Tunaamini washiriki watatoka hapa wakiwa wameimarika na watatekeleza majukumu yao kwa ufasaha kwa maslahi ya wananchi,” amesema Joyce Mushi.

Robhi Richard Wambura, Afisa Mtendaji wa Kata ya Roche, ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo. Amemshukuru Rais Samia na Wizara ya Katiba na Sheria kwa mpango huo, akisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha uwajibikaji na usimamizi bora katika vituo vya kazi.

“Mwanzoni ilikuwa changamoto; unaweza kutoa maamuzi ambayo yanaweza kuonekana kama unamuonea mwananchi, lakini sasa tumejifunza njia bora za kushughulikia changamoto bila shida yoyote,” amesema Robhi Richard.

Elimu ya utawala bora na uraia inaendelea kutolewa katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Mara, na inatarajiwa kufanyika katika halmashauri zote za mkoa huo. Mafunzo haya yameibua matumaini ya kuimarisha uwajibikaji na utendaji bora katika sekta za umma.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!