Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Herry James, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, amefungua rasmi mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Usalama za Mkoa wa Iringa juu ya elimu ya uraia na utawala bora, mafunzo yanayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku tatu yaliyozinduliwa rasmi tarehe 11 Desemba, 2024 mkoani Iringa, Bw. James amewashukuru waandaaji na washiriki wa mafunzo hayo kwa kujitokeza kwa wingi ambapo amesisitiza umuhimu wa mafunzo katika kuongeza uelewa wa masuala ya demokrasia, haki za binadamu, utawala bora, na majukumu ya vyombo vya ulinzi na usalama.
“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo viongozi katika ngazi mbalimbali za utawala ili kuhakikisha tunazingatia misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na demokrasia kwa vitendo,” amesema.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa mafunzo haya yanahusisha wajumbe wa Kamati za Usalama za Mkoa na Wilaya, baadhi ya wataalamu wa halmashauri, na watendaji wa kata zote za mkoa wa Iringa. Pia ameeleza kuwa mafunzo ya ngazi ya halmashauri yatafanyika kwa Kamati za Usalama za Wilaya, wataalam, na watendaji wa kata.
Baadhi ya changamoto zinazokabili mkoa wa Iringa ni pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya haki za binadamu, mila na desturi kandamizi, vitendo vya ukatili wa kijinsia, pamoja na imani za kishirikina. Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kushirikiana kutatua changamoto hizi kwa kushirikisha maarifa watakayopata.