Shilingi milioni 23,540,000 zimetolewa kwa walimu wa shule za sekondari Mtwara Ufundi na Shangani sekondari zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuhakikisha wanafunzi wanapata matokea mazuri na wameombwa kuendelea kuwafundisha wanafunzi kwa bidii na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hao.
Fedha hizo zimetolewa wakati wa ghafla ya kuwapongeza na kutambua mchango mkubwa unaofanywa na walimu kwa kuendelea kuleta matokeo mazuri ya kidato cha nne kwa mwaka 2024,2025 katika manispaa hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyoambatana na utoaji wa vyeti vya pongezi kwa walimu wa shule hizo Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mwalimu Hassan Nyange amesema kipaumbele cha kwanza kwake ni elimu na utaratibu huo utakuwa endelevu kadri ambavyo Mwenyezi Mungu atavyowapatia nafasi ili waipe heshima sekta hiyo ya elimu pamoja na walimu kwa ujumla.
Ameongeza kuwa lengo la manispaa hiyo ni kuhakikisha inaondoa daraja sifuri na kuongeza ufaulu pia amewaagiza walimu wote wa shule za sekondari kuhakikisha wanamaliza kufundisha kabla ya June,2025 ili kuwawezesha wanafunzi kupata muda mwingi wa kufanya mazoezi.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amewataka walimu kutoka shule mbalimbali za sekondari katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuhakikisha wanazingatia mikakati yote waliyojiwekea ili kuendelea kuleta matokeo mazuri kwa watoto wao.
Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kuboresha miundombinu ya shule inayopolekea walimu hao wakawa na mazingira mazuri ya kufundisha.
Baadhi ya walimu hao akiwemo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi, Riyadhi Abubakar amesema watahakikisha wanaendelea kuleta matokeo mazuri kwasababu wanapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa uongozi wa manispaa hiyo.