Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadongosa amesema huduma za usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR inatarajia kuanza mwezi Aprili 2025 kufuatia kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo yaliyowasili nchini Desemba 2024.
Kadogosa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Jumamosi Machi 22, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema Manufaa ya uendeshaji wa Reli ya SGR ni kupatikana kwa usafiri na usafirishaji wenye staha na gharama nafuu, upunguza muda wa safari, uendeshaji wa reli ya SGR bila ruzuku ya Serikali, kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi na upatikanaji wa ajira ambapo ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,880 zisizo za moja kwa moja zimezalishwa kupitia miradi hii.
Aidha, ameongeza kuwa jumla ya thamani ya mikataba iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya SGR ni takribani Dola za Marekani Bilioni 11.6 sawa na Trillioni 29.580.
“Ujenzi wa reli ya SGR kwa awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam hadi Mwanza wenye jumla ya kilometa 1,596 umegawanyika katika vipande vitano (5), hadi Februari, 2025, kipande cha sita, Tabora – Kigoma (Km 506) ujenzi umefikia asilimia 7.81 na kipande cha saba na nane, Uvinza – Malagarasi – Musongati (Km 282) ununuzi wa Mkandarasi na msimamizi wa mradi umekamilika na Mkataba umesainiwa tarehe 29 Januari 2025,”
“Vipande vya Kaliua – Mpanda – Karema (Km 317) pamoja na Isaka – Rusumo – Kigali; upembuzi yakinifu na usanifu wa awali umekamilika na hatua ya utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande hicho zinaendelea,” Ameongeza Kadogosa
Hata hivyo Kadogosa ameendelea kufafanua kuwa Sekta ya uchukuzi hususan kwa njia ya reli ni moja ya kichocheo cha kukuza uchumi na ni chanzo cha kuongeza mapato ya Taifa kwa njia moja au nyingine.
“Faida zingine ni, utunzaji wa mazingira ambapo takribani tani 14,327.3 za hewa ya ukaa zimepungua, kusafirisha mzigo mkubwa kwa mara moja ambapo treni moja itabeba kiasi cha tani 3,000 kwa wakati mmoja, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kupungua kwa gharama za matengenezo ya barabara kutokana na mzigo mkubwa kusafirishwa kwa njia ya reli, kuchangia ufanisi wa bandari na ukuaji wa sekta zingine pamoja na kuchagiza ukuaji wa miji katika maeneo yaliyopo katika ushoroba wa reli,” Ameeleza kadogosa