Wagonjwa zaidi ya 800 wenye matatizo mbalimbali wamejitokeza katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime hadi Februari 26, 2025, ili kupata huduma kutoka kwa madaktari saba bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara – Mwalimu Nyerere.
Akizungumza na Jambo TV, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Yonam Charles, alisema kuwa mwitikio wa wananchi ni mkubwa, kwani ndani ya siku tatu tangu Februari 24, jumla ya wagonjwa 820 wamejitokeza kupata huduma za vipimo na matibabu.
Huduma hizo zinatolewa na madaktari bingwa wa fani mbalimbali, wakiwemo daktari bingwa wa macho, daktari bingwa wa upasuaji wa pua, kinywa na masikio, daktari bingwa wa uzazi, daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, daktari bingwa wa wanawake, pamoja na daktari bingwa wa watoto.
Dk. Charles alisisitiza kuwa zoezi hilo litadumu kwa siku sita na linatarajiwa kufikia tamati Machi 1, 2025. Aliwahimiza wananchi kujitokeza mapema ili kuepuka msongamano wa siku za mwisho. “Lengo letu ni kuwasogezea wananchi huduma kwa gharama nafuu, tofauti na wangepaswa kwenda kupata matibabu katika hospitali nyingine za rufaa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa madaktari hao, Dk. Elias Godfley, ambaye ni daktari bingwa wa mifupa, alisema kuwa ndani ya siku tatu za kwanza, amepokea wagonjwa 150 na kuwafanyia upasuaji, wakiwemo wagonjwa kutoka wilaya jirani kama Rorya.
Baadhi ya wagonjwa waliopata huduma wameeleza kuridhishwa na utaratibu huo. Deus Kituo, ambaye alipata ajali na kuvunjika mguu miaka kadhaa iliyopita, alisema kuwa alifika hospitalini kupata uchunguzi zaidi na amefurahishwa na huduma anayopata.
Dickson Magiga, mtoto wa miaka 12 aliyepata ajali na mkono wake kupinda, alikuwa kwenye foleni akisubiri huduma akiwa na baba yake, Maginga Mete, ambaye alisafiri kutoka Kijiji cha Kikomori, Kata ya Susuni, Tarime Vijijini.
Zoezi hilo linaendelea, na wananchi wanahimizwa kujitokeza kabla ya muda wake kumalizika Jumamosi, Machi 1, 2025.