Mkoa wa Mtwara una jumla ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani zaidi ya 90 ambapo asilimia kubwa inaonyesha kuwa ni watoto wakiume.
Hayo ameyaeleza Aprili 11,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala kwenye Mdahalo ulioandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum uliofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yatatyofanyika kitaifa Aprili 12, 2025 mkoani Mtwara.
Amesema kuwa takwimu hiyo ni ile ya watoto ambao waliofikiwa ingawa anaamini ya kuwa wapo watoto ambao hawajafikiwa na hawapo kwenye takwimu hiyo.
Ameongeza kuwa miongoni mwa changamoto inayopelekea uwepo wa watoto hao katika mkoa huo ni kuwepo kwa talaka holela ambazo zimekuwa sababu kubwa ya watoto kukosa malezi yaliyo bora na baadhi ya watoto kupelekwa kwa bibi ambae nae anahitaji kuhudumiwa na baadhi ya familia kutoipa elimu kipaumbele.
Hata hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo na kutambua umuhimu wa mtoto kwa mkoa na taifa kwa ujumla, mkoa umechukua hatua ikiwemo ya kuwaunganisha watoto kwenye huduma za marekebisho ya tabia, kuwapeleka kwenye vituo vya kulelea watoto pamoja na kuwaunganisha watoto na familia zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Saidi Nyengedi alisema uwepo wa watoto hao ni kosa la wazazi kwa kutozingatia umuhimu wa malezi kwa watoto hivyo wazazi watakapozingatia umuhimu wa malezi hakuna mtoto atakae ishi na kufanya kazi mtaa.
“Mimi nakataa wazazi wanaonyooshea vidole kwa kusema watoto wa sikuhizi, mimi nasema wazazi na walezi wasikuhizi ndio wenye matatizo mana wao wakichukua jukumu lao hapatakuwa na mtoto wa mtaani, mtoto aliyetelekezwa wala siyo unyanyasaji wa kijinsia ila tatizo tunalo sisi wazazi.”Amesema Nyengedi
Nae Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk. Doroth Gwajima alisema mdahalo huo ni nia njema ya serikali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ufumbufuzi unapatikana wa kuhakikisha unatokomeza changamayo ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani.
Pia amewataka wananchi kuwatumia vizuri Maofisa Maendeleo ya Jamii ili kupata suluhu ya migogoro mbalimbali inapojitokeza kwenye familia.
Pia amewataka kutoa taarifa kwa maofisa hao ili aweze kutumia weledi wake kwa ajili ya kukabiliana na taarifa aliyoipokea.
Aidha Gwajima amewataka wazazi wanapofikia hatua ya kuachana kuwatumia Maofisa Ustawi wa Jamii ili waweze kukaa mezani na kupata muafaka wa malezi kwa watoto huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni ‘Imarisha Ushirikiano Kuzuia Watoto Kuishi Mtaani.
Mdahalo huo umewakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini,taasisi binafsi,Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na wananchi lengo ni kujadili vyanzo vya uwepo wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani na kutafuta suluhu ya kudumu kutokana na changamoto hiyo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Imarisha ushirikiano kuzuia watoto kuishi mtaani.