Tarehe 13 Desemba 2024, Umoja wa Wazawa wa Dodoma (Dodoma Legends) umekabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati wa jiko la wafungwa wanawake katika Gereza la Isanga, jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Dodoma Legends, Ahmad Taufiq, ameihimiza jamii kuwakumbuka watu waliopo magerezani kwa kuwapatia misaada mbalimbali. Amesisitiza kuwa uwepo wa wafungwa magerezani ni sehemu ya kupatiwa mafunzo na kurekebishwa tabia, hivyo wanastahili kuungwa mkono.

“hawa ni wanafunzi kama wanafunzi wengine, tuliona umuhimu wa kuja kuwaona, lengo hasa kujua kitu wanachokihitaji. hapa wamekuja kwenye kufundishwa, kwahiyo tusiwachukulie kwenye negative kwamba hawa ni wakosaji tu, hata mtoto akikosea nyumbani unamrekebisha baadae anakaa kwenye mstari ulionyooka” amesema Ahmad
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Zephania Nelingwa, ambaye pia ni Mkuu wa Gereza la Isanga, amepongeza juhudi za Dodoma Legends na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia. Amesema kuwa kuhudumia wafungwa ni sehemu ya ibada na ni mchango muhimu kwa maendeleo ya jamii.

“Kwa niaba ya wanafunzi wetu ambao ni wafungwa na mahabusu nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wana legends kwaajili ya zawadi hizi ambazo zinakwenda kubadilisha miundombinu kwenye gereza Kuu la Isanga Dodoma hasa katika maboresho ya majiko yetu ambayo hivi sasa yameanza kutumia nishati safi.” Ameeleza Kamishna Msaidizi huyo
Vifaa vilivyokabidhiwa vitasaidia kuboresha hali ya jiko la wafungwa wanawake, hatua ambayo inalenga kuboresha mazingira na ustawi wa wafungwa hao.
