Latest Posts

PPRA: SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA TUMEWEKA UPENDELEO KWA WANAWAKE WENYE KAMPUNI

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), CPA Salmin Malole, amesema wanawake bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kupata fursa za kiuchumi, jambo lililoifanya sheria ya ununuzi wa umma kutoa upendeleo maalum kwa kampuni zinazomilikiwa na wanawake ili kuwasaidia kushiriki katika mchakato wa zabuni za umma.

CPA Malole amebainisha hayo Alhamisi Agosti 7,2025 jijini Dodoma wakati wa semina ya kuwajengea uwezo makundi Maalumu. Malole amesema serikali kupitia PPRA imeweka mkazo kwenye ushiriki wa makundi maalum kwa kuwa ni njia ya kukuza uchumi jumuishi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na PPRA, hadi sasa jumla ya vikundi maalum 642 vimesajiliwa katika Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma (NEST). Kati ya hivyo, vikundi vya vijana ni 384 (asilimia 60), wanawake 224 (asilimia 35), watu wenye ulemavu 7 (asilimia 1), na wazee 38 (asilimia 4)

“Mpaka sasa idadi ya tuzo za mkataba zilizotolewa kwa makundi maalum ni jumla ya tuzo mia tano tisini na mbili (592) zenye thamani ya tsh.  bilioni  18.9  kati ya hizi Makundi ya  vijana yamepata tuzo za mkataba 339 zenye thamani ya bilioni  9.3 sawa na 49.3% , makundi ya wanawake yamepata tuzo za mkataba 208 zenye thamani ya Bil 8 sawa na 42.4%, makundi ya watu wenye ulemavu yamepata tuzo za mkataba 18 zenye thamani ya milioni  191 sawa na 1% na makundi ya wazee yamepata tuzo za mkataba 27 zenye thamani ya bilioni 1.4 sawa na 7.2%”.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji katika Ununuzi na Ugavi wa PPRA, Winfrida Samba, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia vijana wanaosomea fani za ufundi na biashara, ili kuwapa maarifa ya kisheria na mbinu za kujisajili katika mfumo wa ununuzi wa umma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi VETA Dodoma, Deodatus Orotha, amesema ushirikiano kati ya VETA na PPRA ni fursa muhimu kwa vijana wanaohitimu ili waweze kutumia mafunzo yao kwa vitendo, hasa kwenye maeneo ya kuandaa zabuni, kujisajili kwenye mfumo wa NEST, na hatimaye kuajiri au kujiajiri.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ushiriki wa makundi maalum katika zabuni za serikali, sambamba na kuongeza uelewa wa matumizi ya mfumo wa NEST kwa wadau wa sekta ya ununuzi na ugavi nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!